Rais wa Marekani Donald Trump ameionya Iran kwamba itaharibiwa iwapo vita vitazuka kati ya mataifa hayo mawili.
''Iwapo Iran inataka kupigana, huo nduo utakuwa mwisho rasmi wa taifa hilo'' , alisema katika ujumbe wa Twitter siku ya Jumapili. ''Musijaribu kuitisha Marekani tena''.
Marekani imepeleka meli za kivita na ndege katika eneo la mashariki ya kati katika siku za hivi karibuni.
Ujumbe huo wa Twitter wa bwana Trump unaadhimisha kubadilika kwa msimamo baada ya jaribio la hivi karibuni la kuficha uwezekano wa vita kati ya mataifa hayo mawili.
Siku chache zilizopita Rais huyo aliwaambia washauri wake kwamba hapendelei shinikizo la Marekani dhidi ya Iran kubadilika na kuwa vita.
Na alipoulizwa na waandishi wa habari siku ya Alhamisi iliopita iwapo Marekani ilikuwa ikijiandaa kivita, Rais Trump alijibu: Sidhani.
Iran pia imepinga madai ya kuwepo kwa hali ya wasiwasi. Siku ya Jumamosi waziri wa maswala ya kigeni wa taifa hilo Javad Zarif alisema kuwa hakuna hamu ya Vita.
''Hakutakuwa na vita kwa kuwa hatutaki vita na hakuna mtu ambaye anafikiria kuivamia Iran katika eneo hili'', Mohammed Javad Zarrif aliambia chombo cha habari cha Irna.