Ikiwa upanuzi wa barabara ya Bagamoyo ukiwa unakwenda kwa kasi hivi sasa, wafanyabiashara wadogowadogo waliokuwa wakifanya biashara eneo la Mwenge jijini Dar es salaam, wameibuka na kulalamikia vitendo vya rushwa kuhusika katika uvunjwaji wa vibanda vyao.
Hayo yameelezwa ikiwa ni wiki ya pili tangu walipovunjiwa vibanda vyao na kuamrishwa na Mkuu wa Wilaya kuhamia katika eneo maalum lililotengwa.
Wakizungumza na www.eatv.tv, baadhi ya wafanyabiashara hao wamesema kuwa wamiliki wa maduka Mwenge wamekuwa wakiwahujumu kwa muda mrefu kwa kutoa rushwa kiasi cha kupelekea maafisa wa TANROADS kuharakisha uvunjwaji wa vibanda hivyo, ili waondoke.
Mjasiriamali, Deodatus Masili Bilanga amesema, "mwanzo wa kuvunjwa kwa vibanda hivi, Serikali ya mtaa haikuhusishwa kwa sababu hawajaja kwetu sisi kama watu wao kutuambia kuwa kuna suala kama hili. Uongozi wetu wa soko umevunjwa na kuvunjwa kwake kuna mazingira fulani, kwa sababu walikuwa imara hadi kwa mkuu wa mkoa walikuwa wanafika, lakini wakakutana na kashikashi nyingi hadi panavunjwa hapa walikuwa wamewekwa ndani."
Kwa mujibu wa wajasiriamali hao, baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mh.Daniel Chongolo kuvunja uongozi wa soko hilo, hawana msemaji yeyote wa matatizo yao na sehemu waliyopelekwa haina mahitaji muhimu kama maji na vyoo, hali inayopelekea kuwepo kwa hatari ya mlipuko wa magonjwa kama Kipindupindu.
Naye mjasiriamali anayejihusisha na biashara ya mihogo, Bi Joyce Yoyo mkazi wa Goba amesema alikuwa na kibanda chake lakini kimebomolewa, hali inayompelekea kufanya biashara juani na kwamba wafanyabiashara wengi wanashindwa kwenda mahali walikoelekezwa kwa sababu ni sehemu ambayo imekaa pembeni na hakuna watu wengi.
Kwa upande wake, ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kupitia kwa msaidizi wake, amesema kuwa ardhi ni mali ya serikali na wafanyabiashara wamepangiwa mahali pa kwenda, hawapaswi kuhoji maamuzi hayo.