KUNA baadhi ya watu kusafiri mara kwa mara siyo ishu sana, lakini kwa upande wa mrembo wa sinema za Kibongo, Jacqueline Wolper Massawe, safari zake zimeshtua wengi, Risasi Mchanganyiko limedokezwa.
Mrembo huyo safari zake zimeshtua kutokana na jinsi ambavyo amekuwa na idadi kubwa ya picha za mara kwa mara anazotupia akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Instagram na kurasa nyingine, wadau mbambali walirudia kuziposti (re-post) huku kila mmoja akieleza la kwake kuonesha kushtushwa kwake.
“Mh! Haiwezekani, angalia hizi picha alizoziposti mwishoni mwa wiki (iliyopita), juzi tena akaposti na leo kaposti, jamani hata kama ni jeuri ya pesa kiasi gani, hii haiwezekani,” alichangia mmoja wa wafuasi wake wapatao milioni 4.3. Mwingine alikwenda mbele zaidi, kwa kuhoji kuwa isije ikawa mrembo huyo anakwenda tu kupiga picha uwanjani hapo akiwa na mabegi yake ya nguo kisha hasafiri.
“Jamani isije mkawa mnaona anaposti tu picha airport (uwanja wa ndege) kumbe hasafiri maana haya mambo wasanii nao hawashindwi,” alichangia mfuasi mwingine. Mbali na hao, wengine walihoji zaidi kuhusu safari hizo kwa kutaka kujua ni nini kinampeleka huko China anakodaiwa kwenda mara kwa mara.
Walihoji anapata wapi pesa za kusafiri mara kwa mara wakati kazi ya uigizaji kwa sasa hailipi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. “Bongo Movies ya sasa kama unavyoona, sasa huyu dada atakuwa anapata wapi pesa hizi za kusafiri kila siku?” Alihoji mfuasi anayejiita Kitoi katika Mtandao wa Instagram.
Risasi Mchanganyiko lilifanya jitihada za hali na mali kumpata Wolper ili aweze kuzungumzia picha hizo na safari zake, lakini hakupatikana kirahisi. Hata hivyo, mtu mmoja wa karibu na Wolper aliyeomba hifadhi ya jina alisema anavyomjua Wolper picha anazoweka mara kwa mara huwa si za wakati husika na hicho ndicho kinachowachanganya watu washindwe kumuelewa.
“Wolper hizi safari unaweza kuta kasafiri kwa miezi tofauti mwaka jana au hata mwaka juzi halafu akawapostia mfululizo leo na watu wakashindwa kuelewa,” alisema mtu huyo. Hata hivyo, gazeti hili linaendelea na jitihada za kumpata Wolper ili lkupata undani wa safari zake za China.