MSHAMBULIAJI wa Simba, Adam Salamba ameomba radhi kwa kitendo cha kuomba viatu kwa staa wa Sevilla, Éver Banega na kudai anakwenda kuvitengenezea fremu kama kumbukumbu.
Mashabiki mbalimbali kuanzia juzi usiku walimnanga Salamba kwa kitendo cha kuomba viatu kwa Banega mara baada ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar na mchezo kuisha kwa Sevilla kushinda mabao 5-4.
Mechi iliandaliwa na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportPesa. Katika picha ya video ambayo ilisambaa mitandaoni inaonyesha Salamba akizungumza jambo na Banega raia wa Argentina na baadaye akaonyesha kwa ishara kisha staa huyo kutoka La Liga akainama na kufungua kamba za viatu vyake.
Kitendo hicho kilionekana kuwashangaza wengi kwani haijazoeleka kuonekana mchezaji akiomba viatu zaidi ya jezi lakini Championi tunaona ni jambo la kawaida kutokea kwa wanamichezo. Hata hivyo baada ya kukabidhiwa viatu hivyo Salamba aliviposti vikiwa na vingine saba kwenye mtandao wake wa Instagram na kuomba radhi kwa wote waliokwazika kwa kitendo hicho.
Championi lilifanikiwa kuzungumza na salamba kuhusiana na ishu hiyo ambapo alianza kwa kusema: “Nichukue nafasi hii kuwaomba radhi wale ambao wamekwazika kutokana na jambo lile lakini kwangu ni kitu kikubwa kwa sababu nikiwa mchezaji kijana natamani kuona nakwenda kucheza nje.
“Sasa nimepata fursa ya kucheza na Sevilla ambayo watu wengi wameitamani lakini hawakuipata ndiyo maana niliamua kuomba viatu kwa ajili ya kumbukumbu ya kizazi changu huko mbele maana kama viatu ninavyo vya kutosha ila vile nitavijengea fremu kwa ajili ya kumbukumbu tu,” alisema Salamba.