Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu waongeze kasi ili utendaji kazi serikalini uweze kufikia hatua nzuri.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo alipokutana na viongozi na watumishi wa ofisi yake na kufuturu nao pamoja kwenye makazi yake jijini Dodoma.
“Ninawashukuru watumishi wote kwa ushirikiano mnaotupatia mimi pamoja na mawaziri wenzangu, makatibu wakuu wote watatu, Wakurugenzi mbalimbali na wakuu wa vitengo. Tunatakiwa tuongeze kasi ili tufikie hatua nzuri ya utendaji kazi serikalini”,amesema Waziri Mkuu
Aidha amesema utendaji kazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu ni mgumu kwa sababu unahusika na usimamizi wa shughuli za Serikali nzima na watendaji wote wa Serikali.
"Sekta yetu ni ngumu kwa sababu sisi ni wasimamizi wa Serikali na watendaji wote wa Serikali. Tuna wajibu wa kuwaunganisha watendaji wa wizara zote serikalini”, ameongeza Waziri Mkuu.
“Sisi sote ni watumishi wa umma, kwa hiyo mchango wenu una maana kubwa na unachangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Serikali nzima. Ninawapongeza kwa utumishi mwema na wenye uadilifu”.amesema Waziri Mkuu