Serikali Yashauriwa kutowapuuza wawekezaji wanaotoka China


Serikali  imeshauriwa kutowapuuza wawekezaji wanaotoka China na kuja kuwekeza badala yake wawatumie kama daraja la kuweza kufikia malengo ya kuwa nchi yenye uchumi mkubwa duniani.

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda,   alipokuwa katika ghafla ya uzinduzi wa  pombe kali aina ya Moutai ambayo kiwanda chake kipo China.

Alisema pamoja na uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na China, lakini bado wameamua kutafuta kila mbinu ili kuweza kushirikiana katika masuala ya kiuchumi.

“Ushirikiano uliopo baina yetu na China ni jambo kubwa, tuendelee kuukuza, wao kama nchi wameamua kutafuta kila mbinu ya kushirikiana na nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, hivyo tunapaswa kutumia nafasi hii ambayo wawekezaji hawa wameamua kutupa kama daraja kufikia malengo tunayoyataka kama nchi,” alisema.

 Pinda alisema China ni taifa la pili kwa ukuaji wa uchumi duniani, hivyo hawapaswi kupuuzwa wanapokuja na mawazo yao ya kuanzisha biashara.

Alisema wawekezaji wa China wameamua   kutangaza biashara zao kubwa nchini, ikiwamo pombe hiyo ambayo ni maarufu  China na nchi za Afrika Magharibi.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi na Naibu Katibu wa Bodi ya Moutai, Wang Yan, alisema miaka 40 iliyopita China ilikuwa miongoni mwa mataifa masikini duniani kuliko umasikini uliopo katika baadhi ya nchi za Afrika.

Alisema kwa sasa kampuni zilizoanzishwa nchini humo zimefanikiwa kubadili mfumo wa maisha ya Wachina na kupata mafanikio makubwa ya kibiashara na kuchangia kuleta maendeleo kwa haraka.

“Sisi kama Moutai, tumechagua Afrika kutokana na kuwa na ushirikiano mzuri katika kipindi kizuri kilichopita na ushirikiano huu unaonekana utazidi kuimarika katika siku zijazo na kuongeza mafanikio,” alisema.

Alisema mwaka jana mapato ya kampuni zilizopo chini ya kampuni mama ya Moutai Group yalikuwa ni Dola za Marekani bilioni 12.6, faida halisi ilifikia dola bilioni 5.8 na mapato ya kodi yalikuwa ni dola bilioni 5.6 na iliweza kumiliki mali zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 30.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad