Serikali imesema watumishi wa umma hawapaswi kuomba nyongeza ya mwaka ya mshahara, bali Serikali ndiyo yenye uamuzi wa kutoa au kutotoa nyongeza.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na utawala bora) Dk. Mary Mwanjelwa
Hayo yamesemwa bungeni na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na utawala bora) Dk. Mary Mwanjelwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Tunza Issa Malapo (CHADEMA).
Mbunge huyo alitaka kujua serikali inatumia sheria ipi kutowapa wafanyakazi stahiki zao zinazohusu kupandishwa madaraja, na ongezeko la mwaka.
"Kwa mujibu wa kanuni E.9 (1) ya kanuni ya kudumu katika utumishi wa umma ya mwaka 2009, toleo la tatu, nyongeza ya mwaka ya mishahara haipaswi kuombwa", amesema Dk. Mwanjelwa
Ikumbukwe kuwa katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, Mei mosi, ambayo kitaifa yalifanyika Mkoani Mbeya na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye alisema kuwa hatoongeza mshahara mwaka huu, kwani ahadi yake ya kupandisha mishahara katika uongozi wake haijaisha kwa sababu bado hajamaliza muda wake madarakani.