Uongozi wa klabu ya Simba umezungumzia tetesi za mshambuliaji wake, Meddie Kagere anayehusishwa kujiunga na miamba ya soka nchini Misri, klabu ya Zamalek.
Kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Crescentius Magori, ameeleza kuwa mpaka sasa hakuna ofa yoyote iliyotolewa na timu yoyote juu ya mshambuliaji huyo.
Magori amesema hawana ofa yoyote iliyofika mezani kwa ajili ya Kagere kutakiwa na badala yake wamekuwa wakisikia stori ambazo si rasmi, huku akiwataka wenye nia ya kumtaka Kagere walete ombi lao kwa maandishi na waweze kukubaliana juu ya usajili wa straika huyo.
"Hakuna ombi lolote lililokuja mezani kuhusiana na Kagere kusajiliwa kutoka klabu yetu ya Simba, ni taarifa tu za mitandaoni ambazo si rasmi zimekuwa zikiandikwa", amesema Magori.
"Kama kweli wana dhamira na wanamtaka mchezaji, si Zamalek tu hata wengine, wanapaswa kuja na tutazungumza na si matamko ya mitaani huko", ameongeza.
Simba iko mkoani Morogoro, ambapo hii leo inatarajia kucheza mchezo wake wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania bara dhidi ya wenyeji Mtibwa Sugar katika uwanja wa Jamhuri. Katika mchezo huo, Simba itakabidhiwa kombe lao la ligi 2018/19 baada ya kuibuka mabingwa kwa mara ya pili mfululizo.