MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Temeke ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mtoni, Bernard Mwakyembe, amepangua tuhuma nzito alizozitoa mwanachama na kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagari maarufu kama Mdude Chadema, akidai kuwa alitekwa na vyombo vya usalama.
Mwakyembe ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, amesema watu aliomteka Mdude ni wa Chadema wala si vyombo vya usalama kama alivyodai hivi karibuni baada ya kupatikana.
Diwani huyo amesema wapo vijana mbalimbali wa Chadema ambao amedai waliwahi kutekwa na kikundi maalum ambacho kipo ndani ya Chadema, ambacho kimekuwa kikitumika kuwateka na baadaye wakishaachiwa wanaambiwa wavitaje vyombo vya usalama ndivyo vinawateka kwa kuagizwa na rais.
Aidha, Mwakyembe ameongeza kuwa vyama vya upinzani vimekuwa vikitumika na mabeberu pamoja na mafisadi ambao hawapendi maendeleo anayoyafanya Rais Magufuli, hivyo kuwatumia ili kupotosha ukweli. Ameongeza kwamba kwa sababu aliwahi kuwa ndani ya chama hcho, anafahamu mbinu zote wanazotumia na propaganda wanazofanya kuwahadaa wananchi.
Ameendelea kusema kwamba Rais Magufuli ana mambo mengi ya kufanya kwa ajili ya wananchi wake, wala hawezi kushughulika na mtu badala yake anashughulikia matataizo ya wananchi waliomweka madarakani.
“Wapo wakosoaji wakubwa tunawafahamu akina Maria Sarungi, Fatuma Karume, mbona hawajawahi kutekwa? Atekwe yeye Mdude ni nani? Eti anasema kutekwa kwake kumetokana na ziara ya rais, huo ni uongo mkubwa, waliomteka Mdude ni Chadema wenyewe,” amesema