UMOJA wa Wazalishaji wa Mifuko Mbadala Nchini imewaondoa hofu Watanzania na kusema kuwa vipo viwanda vya kutosha vya kuzalisha mifuko hiyo hapa nchini na hivyo kuweza kutosheleza mahitaji ya soko ya bidhaa hiyo ifikapo Juni Mosi, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari leo Jumatano (Mei 22, 2019) Jijini Dar es Salaam kuhusu Mipango na Mikakati ya Umoja huo katika uzalishaji wa mifuko mbadala nchini, Mwakilishi wa Umoja huo Allan Ngumbuke alisema Watanzania hawana budi kubadili mtazamo kuhusu matumizi ya mifuko ya plastiki inayoisha matumizi yake Mei 31, mwaka huu.
Aliongeza kuwa mara baada ya Serikali kutoa Tamko kuhusu Katazo la Mifuko ya plastiki ifikapo Mei 31, mwaka huu na kuanza kutumika kwa mifuko mbadala kuanzia Juni Mosi, mwaka huu Umoja huo walijipanga kikamilifu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu na mafunzo mbalimbali, ili kuwafanya Watanzania kuona kuwa mifuko mbadala ni sehemu ya kujiongezea kipato.
“Baada ya katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki, wazalishaji wa mifuko mbadala wameongeza kasi ya uzalishaji na wengi wameshaagiza mashine zipo njiani kuja na nyingine zinatengeneza mifuko mbadala, mfano hai ni Tanpak Tissue Paper Ltd, Hanpal, Green Earth Paper Products Ltd, Harsho Group” alisema Ngumbuke.
Kwa mujibu wa Ngumbike alisema uzalishaji wa mifuko mbadala utaibua viwanda vingi vya nyumbani, kwani teknolojia yake ni rahisi na pia mifuko hiyo inayozingatia utunzaji wa mazingira ipo ya aina nyingi na itakuwepo ya kutosha kuendana na mahitaji ya soko na ukuaji wa uchumi na hivyo kuendelea kuhudumia soko la ndani na nje ya nchi.
Aidha Ngumbuke aliwataka wadau na wananchi wanaotaka kuwekeza kwenye mifuko mbadala kuwa zipo malighafi za kutosha zinayopatikana katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kwa malighafi ya karatasi inayopatikana katika viwanda vya Mufindi Paper Mills Ltd na Tanpak Tissue Ltd wakati kwa upande wa malighafi ya vitambaa laini zitapatikana katika cha kiwanda cha Harsho Group kilichopo Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
“Tunaiomba Shirika la Viwanda Vidogovidogo Nchini (SIDO) waweke kipaumbele na viatamizi vya uzalishaji wa mifuko mbadala kwa kuwa SIDO ipo nchi nzima na ni mahiri kwa kutoa mafunzo ili washiriki wake wataleta matokeo chanya na makubwa kwa haraka zaidi” alisema Ngumbuke.
Kwa upande wake Afisa Tawala wa Kiwanda cha Tanpak Tissue Ltd, Michael Mjungu alisema kiwanda chake kimejipanga kikamilifu kuzalisha malighafi za kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa mifuko hiyo na kuwataka wafanyabiashara kuondoa hofu kuhusu uwezo wa viwanda vya ndani ya Tanzania kuweza kuzalisha mifuko mbadala.