VIDEO: Ndugai, mbunge Masele watuhumiana bungeni


Dodoma. Unachoweza kusema ni kuwa taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imewagonganisha Spika  Job Ndugai na mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele.

Hiyo inatokana na taarifa hiyo kuibua  mvutano mkali baina yao bungeni jijini Dodoma  huku kila mmoja akimtuhumu mwenzake.

Hayo yametokea leo Alhamisi Mei 23, 2019 baada ya mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel  Mwakasaka kumaliza kusoma taarifa ya kamati hiyo iliyomhoji Masele aliyekuwa akituhumiwa na Ndugai  kwa utovu wa nidhamu na kugonganisha mihimili ya Serikali katika Bunge la Afrika (PAP) nchini Afrika Kusini.

Mwakasaka amesema Masele ambaye ni makamu  wa Rais wa PAP  alituhumiwa kuchonganisha viongozi, kughushi nyaraka, kudharau wito uliomtaka kurejea Tanzania aliopewa na Ndugai ili ahojiwe kuhusu tuhuma hizo.



Akizungumzia mahojiano kati ya Masele na kamati hiyo yaliyofanyika Mei 20, 2019, Mwakasaka amesema wamependekeza Masele kusimamishwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge kuanzia leo Alhamisi.

Baada ya taarifa hiyo kusomwa,  Ndugai alisimama na kulieleza Bunge kuwa taarifa hiyo imekuwa fupi kwa kuwa kuna mambo ya kulinda hadhi ya Bunge na masuala yanayohusu nchi, hivyo asingewezekana kuweka kila kitu.


Masele ajitetea

Huku akishangiliwa na wabunge wa pande zote, Masele amesema, “Naomba kukuomba radhi wewe (spika) , wewe na familia yako kwa usumbufu wowote ulioupata kupitia sakata hili. Ninawaomba radhi wabunge wenzangu kwa usumbufu mlioupata.”

“Nitumie nafasi pia kuwaomba radhi viongozi wangu wakuu, mwenyekiti wa chama changu Rais John Magufuli, Waziri Mkuu kwa usumbufu wowote walioupata kutokana na jambo hili.”

Ameongeza, “Makosa yangu yaliyoorodheshwa ningefurahi kama hansard (taarifa rasmi ya Bunge) ingeletwa katika Bunge hili ili Bunge na Watanzania wajue.”

Masele ambaye amewahi kuwa naibu Waziri wa Nishati na Masini amebainisha kuwa katika kuhudhuria vikao vya PAP, huwa wanapeleka taarifa baada ya kupokea barua ya mwaliko wa kushiriki mikutano hiyo.

“Utaratibu wa Bunge huwa hatuji kuomba kibali bali tunatoa notification (taarifa) kwa hiyo Spika nilileta taarifa katika ofisi ya Bunge. Tuhuma zinasema nimesafiri bila kibali, sisi tuko wanne (wabunge wa PAP kutoka Tanzania), kwa nini Masele, ninaadhibiwa mimi na si wabunge wengine,” amehoji Masele huku wabunge, wengi wakiwa wa upinzani wakimshangilia.

Amesema uamuzi wa  Ndugai kumuandikia barua Rais wa PAP ya kusimamisha uwakilishi wake katika Bunge hilo ilitaka kutumika kama kigezo cha kumng’oa kwenye wadhifa wake wa makamu wa rais.

“Rais wa PAP alitaka kunivua kwa kutumia barua yako, nilitafakari sana kwa maslahi ya wabunge, Taifa na kijana ninayekua. Nilifikilia haraka kama Spika ananisimamisha bila kunisikiliza ndio sababu ya kukata rufaa kuwasiliana na viongozi wa CCM na Waziri Mkuu.”

“Ninasikitika kwamba sikuchonganisha mihimili, nisingeweza kupeleka jambo hili kwa waziri,” amesema mbunge huyo wa Shinyanga Mjini huku akionyesha barua hiyo.

Akizungumzia video iliyosambaa mitandaoni ikimuonyesha akizungumza katika Bunge hilo lililokuwa likiendelea Afrika Kusini na kumalizika Ijumaa Mei 17, 2019, Masele amesema Rais huyo wa PAP  alitaka kumng’oa katika madaraka na kwamba alitumia barua aliyotumiwa na Ndugai.

“Niliamua kusimama kwa ujasiri kuwa nina support ya Serikali yangu kwani barua hii siitambui. Spika nimekubali mimi ni kijana, nimebeba dhamana ninakuomba radhi. Ieleweke sikufanya kwa makusudi kukuvunjia heshima, kukudharau nilipokea wito wako saa 11 jioni wa kunitaka nifike Dodoma saa 4 asubuhi.”

“Nimekwenda Afrika Kusini bila kupewa nauli, tiketi na ningepata wapi watu wa kulipa bili hotelini. Na wakati huo Rais wa PAP alikuwa na hatia za udhalilishaji wa kijinsia, natambua Rais wa PAP anawasiliana na wewe ili mimi nisirudi PAP, najua mnatumiana barua,” amesema Masele.

Huku kukiwa na hali ya utulivu bungeni, Masele aliongeza, “Naamini umefanya ushauri wa kutosha, nimekubali makosa kwa heshima ya Bunge langu nakuja mbele yako kuomba radhi, nashukuru kwa nafasi yangu Watanzania kujua ukweli.”

Amesema amekuwa mbunge miaka tisa na hajawahi kuitwa katika kamati yoyote ya nidhamu.

“Kwa kutumia kanuni ya 68(1) ya kanuni za Bunge ninaikataa taarifa  iliyosomwa na mwenyekiti Mwakasaka,” ameongeza Masele.

Spika Ndugai

Baada ya Masele kumaliza kuzungumza, Ndugai amesema, “Jambo hili ni la kipekee sana. Bahati mbaya sana Masele haelewi hata hivi sasa kipi kinaendelea. Masele hakuitwa kwa sababu ya jambo lolote kule PAP.”

“Kuna mambo yanafanyika huko na wanaopaswa kutueleza ni wabunge wenzao wa PAP. Tulimwita nyumbani na narudia tena na tena, nikirudia anapeleka katika migogoro.”

Amesema walimuita Masele nyumbani (Tanzania)  kwa kuwa aliwaandikia  viongozi wa juu kabisa ujumbe wa ajabu, “Akigonganisha mihimili na ndio sababu tulimtaka arudi.”

Amesema Masele alipewa barua ya kurejea Tanzania kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Rais wa PAP pamoja na njia ya WhatsApp lakini alikaidi.

“Ameshagonganisha Spika na Rais. Tumekuita kwa sababu ya tabia mbaya. Sababu za PAP ni za kwenu. Japo tunasononeka na tunasikitika. Hata nikiingia huko  huwakilishi taswira za nchini huko, wewe unatupeleka huko.”

“Tatizo lako ni uongo, kugonganisha viongozi, fitina na uchonganishi. Binafsi nimesononeka sana na naendelea kusononeka. Hata wewe huelewi,” amesema Spika Ndugai.

“Ameniambia aombe radhi halafu anasema mengine. Hatujakuita kwa hayo ya PAP, tumekuita kwa haya ya nyumbani. Acha tabia hizo, acha, ujanja ujanja wa kuzungusha maneno, acha.”

Ndugai ataka Bunge kumpuuza Masele

Baada ya maelezo hayo, Ndugai aliliomba Bunge kumpuuza Masele hoja iliyoungwa mkono na wabunge waliosimama na kushangilia kwa mtindo wa kupiga meza huku Masele akiwa ameketi na kugonga meza.

By Ibrahim Yamola, Mwananchi iyamola@mwananchi.co.tz
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad