Wananchi wa Mtaa wa Nyunguu katika Halmashauri ya Mji wa Babati, Mkoani Manyara, wamelalamikia uongozi wa mtaa huo, kuwalazimisha kulipia Sh.10,000 ili waweze kupatiwa Vitambulisho vya Taifa.
Malalamiko hayo waliyatoa jana mjini Babati, kuhusu kadhia hiyo ambayo inaongozwa na ofisi ya mtaa kupitia kwa Ofisa Mtendaji na baadhi ya wajumbe wa serikali ya mtaa.
Mmoja wa wakazi hao, Mustafa Rwamcho, amesema alienda siku moja ofisi ya mtaa huo ili aweze kuchukua kitambulisho chake, lakini alinyimwa kwa madai kwamba anatakiwa achangie mchango wa Shule ya Sekondari Babati Day, Sh. 10,000 ndipo angepewa kitambulisho chake.
“Mimi baada ya kunidai nitoe fedha niliamua kukiacha na mpaka sasa sijarudi tena na sijui itakuwaje, maana hiki kitambulisho kinahitajika, mfano ukienda nje ya nchi unaweza ukatakiwa uonyeshe kitambulisho hicho, ili kuthibitisha uraia wako,’’ amesema Rwamcho.
Aidha, amesema kwa kuwa hali yake kiuchumi haikuwa nzuri, alikiacha kitambulisho hicho huku akisema kuendelea kukikosa italeta madhara zaidi kwa kuwa mamlaka ya mawasiliano inawataka watumiaji wa simu kusajili laini za simu wawe na vitambulisho hivyo.
“Kwa kuwa rais Magufuli alishasema vitambulisho hivi ni bure,namuomba atusaidie kuwawajibisha viongozi wa namna hii, ambao wanatuuzia vitambulisho wakati vinatakiwa kutolewa bila malipo ya aina yeyote,’’ alifafanua.
Mkazi mwingine, Leah Mapinda, alisema anashangaa ofisi ya mtaa, kuwatoza fedha hizo huku akidai mdogo wake alilipishwa fedha hiyo na kusisitiza kuwa endapo wataendelea kuwatoza wananchi ambao baadhi hawana uwezo hawatapata vitambulisho.
Mapinda alihoji waliopewa mwaka jana hawakutozwa Sh.10, 000, lakini mwaka huu viongozi wanaanza kuwatoza fedha hiyo, ilhali ni haki yao kupata Vitambulisho vya Taifa.
Mkazi mwingine Musa Rajab, amesema kuwa viongozi kuwatoza fedha wananchi katika kuwapatia vitambulisho ni kukiuka maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi, Kangi Lugola na rais John Magufuli wanapokuwa kwenye ziara zao.
Kwa upande mwingine, uongozi wa mtaa wa Nyunguu, ulikataa kuzungumzia tuhuma hizo na kutoa masharti ya kuwa na kibali cha kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati.
Naye mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Fortunatus Fwema, amesema uongozi wa kata au mtaa watakuwa wamejiwekea utaratibu huo na kama kuna wananchi wana malalamiko ya kutozwa fedha, wafikishe taarifa ofisini kwake au kwa mkuu wa wilaya.
Wananchi Walalamikia Kutozwa Tsh 10,000/= ili wapatiwe vitambulisho vya Taifa
0
May 01, 2019
Tags