Wataalam Wa Sheria Waitaka Sheria Mpya Ya Kudhibiti Vimelea Hatarishi Nchini

Wataalam Wa Sheria Waitaka Sheria Mpya Ya Kudhibiti Vimelea Hatarishi Nchini
Wataalam wa sheria kutoka katika sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori na mifugo pamoja na mazingira wameshauri kutungwa kwa sheria mpya itakayohusika na  ulinzi na usalama wa  vimelea hatarishi ili kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa sampuli za vimelea hivyo kutoweza kueeneza  magonjwa  kwa binadamu.

Sheria hiyo imeshauriwa kuzingatia dhana ya Afya moja ambayo hujikita katika kujumuisha sekta zote za Afya katika kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayomuathiri binadamu, lengo nikusaidia katika kuimarisha ulinzi na usalama wakati wa kuvichukua  vimelea kwa wanyama, binadamu na mimea  au  wakati wa kuvisafirisha na  kuvipeleka maabara kwa ajili ya Uchunguzi na wakati wa kuviharibu mara baada ya kuvifanyia uchunguzi.

Wakiongea kwa nyakati tofauti wakati wa mkutano wa kujadili masuala ya kisheria ya Ulinzi na Usalama wa vimelea hatarishi, uliofanyika kwa siku tatu na kufungwa leo  tarehe 31 Juni, 2019, Jijini Arusha, kwa pamoja,  wataalam wa sekta za Afya  na wanasheria wa sekta hizo wamebainisha kuwa uwepo wa sheria hiyo utasaidia kuimarisha usalama  na ulinzi kwa wanaohusika na shughuli za vimelea hivyo, mafunzo kwa wataalamu hao, miundo mbinu  ya maabara, pamoja na kuainisha orodha ya vimelea hivyo.

Wataalamu wa sekta za Afya walioshiriki mkutano huo, wamebainisha kuwa, sheria hiyo ni ya muhimu kwa kuzingatia kuwa, Dunia imekuwa na tishio kubwa la magonjwa ya kuambukiza yanayoweza kusambaa kwa muda mfupi na kusababisha madhara makubwa kwa binadamu, mifugo, wanyama pori na kuleta uharibifu wa mazingira. Wamefafanua kuwa,  Tafiti zinabainisha kuwa kila mwaka huibuka magonjwa ambukizi mapya kati ya matano hadi Nane duniani. Hivyo inakadiriwa ifikapo mwaka 2030, dunia itakuwa na magonjwa ambukizi mapya 30.

Aidha, wamebainisha kuwa, Tafiti mbalimbali duniani zinaonesha pia, kuwa asilimia 60% ya vimelea vya magonjwa ambayo huambukizwa binadamu vinatoka kwa wanyama hususani  wanyamapori na baadae kusababisha magonjwa kwa binadamu.Tayari Tanzania kupitia Dhana ya Afya Moja,  imeainisha magonjwa sita ya kupewa kipaumbele ambayo ni; Kimeta, Kichaa cha mbwa, Mafua ya ndege, Homa ya Bonde la ufa, Malale na Ugonjwa wa  kutupa mimba  wanyama.

 Akiongea wakati wa akifunga mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali, Jimmy Matamwe amebainisha kuwa serikali imedhamiria kuijenga jamii ya watanzania yenye Afya bora kwa kuikinga na majanga yatokanayo na magonjwa ya mlipuko,  hivyo ushauri huo wa wanasheria na wataalam wa sekta hizo za afya  utaratibiwa kwa uhakika ili kuweza kuijenga jamii salama.

Tarehe 13 Februari 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua Dawati la Uratibu la Afya moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, likiwa na lengo la kusimamia na kuratibu shughui za Afya moja nchini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad