Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, amesema hatamvumilia askari au mtumishi aliyeopo chini ya wizara hiyo iwapo atabainika anamnyanyasa, kumtishia au kumsumbua mwekezaji anayefuata sheria ikiwamo kulipa kodi.
Lugola amesema hayo jana mjini Morogoro alipozungumza na viongozi wa Kampuni ya Tumbaku ya Tanzania Leaf.
Amesema askari atakayebainika kufanya hivyo sheria dhidi yake itachukua mkondo wake kwani kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wawekezaji kuonewa na baadhi ya vyombo vya ulinzi bila sababu, huku wakitishiwa na kuapa kuwa atakayebainika atamfukuza kazi mara moja.
Pia, amesema hivi karibuni uongozi wa kampuni hiyo uliwasilisha malalamiko kwa ofisi ya Waziri Mkuu kutokana na viongozi wake wakuu kunyanyaswa na kutishiwa kukamatwa na polisi mkoani Morogoro.
Lugola amesema Serikali imedhamiria kufikia uchumi wa kati kwa sekta ya viwanda na kwamba, imetoa nafasi kubwa kwa wawekezaji kuwekeza nchini kwa kufuata sheria zilizopo.
“Lakini kumekuwapo na baadhi ya watumishi ndani ya wizara hii wakiwamo baadhi ya askari kuwabugudhi kwa kutaka kujipatia kipato, sasa niwaonya acheni tabia hiyo,” ameonya Lugola.
Pia, Lugola ameagiza uongozi wa Polisi Mkoa wa Morogoro kumpa taarifa za kina ili kuwachukua hatua kwa waliofanya vitendo hivyo ili wawe mfano kwa wengine.
Awali, Mkurugenzi Mzawa wa Kampuni hiyo, Richard Sinamtwa, amesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali licha ya kampuni hiyo kutoa ajira kwa zaidi ya vijana 10,000 ambao ni wakazi wa Manispaa ya Morogoro.
Amesema moja ya changamoto hizo ni kutishiwa kukamatwa na polisi bila sababu wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa lengo la askari hao kutaka rushwa.