Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), January Makamb amewataka watendaji na watumishi wa mkoa wa Dar es Salaam, kutotumia nguvu kuwapigana virungu wananchi watakaokutwa na mifuko ya plastiki kuanzia Juni Mosi, mwaka huu.
Aidha, amepiga marufuku watendaji watakaosimamia kazi hiyo kutoingia kwenye maduka, ofisi na kwenye magari ya watu kutafuta mizigo ya mifuko ya plastiki.
Waziri Makamba, alitoa angalizo hilo jana, wakati akizungumza na watendaji wa mkoa wa Dar es Salaam, wakiwamo wakuu wa wilaya, makatibu tawala, wakurugenzi, madiwani, wenyeviti na watendaji wa kata na mitaa, wasimamizi wa masoko, maofisa afya, mazingira na biashara kujadili utekelezaji wa marufuku ya mifuko ya plastiki.
“Katika utekelezaji wa sheria hii mpya inayoanza Juni Mosi, mwaka huu, hatutegemei kuona watu wanaendelea kubeba mifuko, lakini pia hatutegemei kuona kinamama wanapigwa virungu na mgambo kisa wamebeba mifuko na wala hatutegemei kuona watu kuporwa mali zao,” alisema Makamba.
Alieleza katika utekelezaji wa sheria hiyo, watendaji watakaosimamia kazi hiyo hawapaswi kuingia kwenye ofisi, maduka na kufungua magari ya watu kutafuta mizigo ya mifuko ya plastiki.
“Tunatarajia hakuna mwananchi ambaye atatumia mifuko ya plastiki kuanzia Juni Mosi, lakini watendaji wanaosimamia kazi hii, hatutarajii kuona wanapita kwenye ofisi, maduka na kufungua magari ya watu kutafuta mizigo ya mifuko hili hatulitarajii kabisa,” alisema Makamba.
Waziri Makamba atoa neno katazo la mifuko Plastiki 'hatutegemei kuona wakina mama wanapigwa'
0
May 22, 2019
Tags