Wizi: Mteja Atimua na Gari la Sh5 Bilioni Bila Kulilipia


Polisi nchini Ujerumani wanamtafuta mtu mmoja ambaye alikuwa mteja mtarajiwa kwa wizi wa gari aina ya Ferrari lenye thamani ya $2.2 milioni (zaidi ya Shilingi bilioni 5 za Kitanzania).

Kwa mujibu wa polisi wa Düsseldorf, mwanaume huyo ambaye alionesha nia ya kulinunua gari hilo aina ya Ferrari 288 GTO aliingia kwenye majadiliano na wauzaji na baadaye kufanya zoezi la kulijaribu gari hilo akiwa na mwakilishi mmoja wa wauzaji hao.

Katika hali isiyotarajiwa, baada ya mwakilishi huyo wa wauzaji kutoka nje ya gari, mteja huyo mtarajiwa alitimua na gari hilo pasipojulikana.

Msemaji wa kampuni ya udalali ya RM Sotheby amekaririwa na gazeti la The Westdeutsche Allgemeine Zeitung akieleza kuwa gari hilo lililoibiwa awali lilikuwa linamilikiwa na dereva wa magari ya Formula 1, Eddie Irvine.

Baada ya msako, gari hilo lilikutwa likiwa limefichwa kwenye gereji moja ndani ya mji wa Grevenbroich kusini mwa Düsseldorf, Jumanne jioni. Polisi wamesema bado wanamtafuta mtu huyo aliyejaribu kuliiba gari hilo.

“Hili ni gari ambalo vigumu sana kuliiba kwa sababu ni vigumu sana kuliuza. Ni kama mchoro maarufu ambao kila mtu anaweza kuutambua haraka akiuona na kutokana na bei yake ni vigumu sana kuiuza kiholela,” alisema Peter Haynes, msemaji wa kampuni hiyo ya udalali.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad