KOCHA Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera amesema kuwa kiungo wake mshambuliaji, Ibrahim Ajibu atafute sababu nyingine iliyomzuia kujiunga TP Mazembe ya DR Congo na siyo dau la usajili.
Kauli hiyo aliitoa ikiwa ni siku chache ziibuke taarifa za dili la Ajibu kushindikana kwa kile kilichoelezwa kushindwana katika dau la usajili ambalo Mazembe walitenga dola 30,000 (zaidi ya Shilingi Milioni 60).
Mara ya taarifa hizo kuzagaa za kushindikana kutua Mazembe zikaibuka tetesi za nyota huyo kwenda Simba baada ya kusaini mkataba wa awali wa miaka miwili huku akitanguliziwa Shilingi Milioni 20.
Akizungumza na Championi Jumatano, Zahera alisema ni ngumu kwa Mazembe kushindwana na Ajibu katika dau la usajili.
“Ninaahidi kufuatilia kwa ukaribu usajili wake na kikubwa kujua dau la usajili alilowekewa mezani na klabu hiyo.”
“Mimi ndiye niliyefanikisha mipango hiyo ya Ajibu kusaini Mazembe, kwani nilimwambia kocha wa Mazembe amenipigia simu kaniulizia kuhusu wewe na uzuri nilimpa taarifa zako zote nzuri nikamuuliza upo tayari kujiunga nayo akanijibu sawa, mimi nikaanza kumuwekea mipango sawa.
“Na baada ya siku chache kweli Mazembe wakatuma barua Yanga ya kumuhitaji Ajibu na baada ya hapo nikawaachia wenyewe waendelee kuwasiliana kati yake, viongozi wa Yanga ambao wanammliki na Mazembe.
“Hadi ninaongea na wewe sijamuona tena katika timu, hivyo sijajua sababu iliyosababisha na nilipouliza nikaambiwa kuwa anaumwa malaria, lakini ninaahidi kufuatilia kwa karibu suala hilo nitajua kama kweli tatizo ni dau la usajili au hofu ya kukaa benchi imesababisha kwani Mazembe ina mastaa wengi
“Mchezaji kama Ajibu anatakiwa kujiongeza katia kupata mafanikio hizi timu kama Simba na Yanga haziwezi kumlipa kama ambavyo angelipwa na Mazembe,” alisema Zahera.
MKUDE NA NDEMLA
Zahera ametamka kuwa hana mpango na viungo wa Simba, Jonas mkude na Said Ndemla ingawa baadhi ya viongozi wanawatamani. Kauli hiyo ameitoa juzi kwenye mahojiano maalum yaliyofanyika kwenye hoteli ya kisasa ya The Atriums Hotel iliyopo Sinza Afrikanasana jijini Dar es Salaam mara alipokutana na Waandishi wa Gazeti hili.
Zahera alisema kuwa, kwa hapa nchini timu alizopanga kwenda kufuata wachezaji kwa ajili ya kuwasajili ni KMC ya jijini Dar es Salaam na Lipuli FC na siyo Simba.
“Katika usajili wangu mpya nimepanga kusajili wachezaji tisa pekee kati ya hao wapo sita kutoka nje ya nchi na watatu wazawa badala ya wawili nilioahidi kuwasajili hivi karibuni.
“Katika usajili wangu hautakuwa na mchezaji yeyote wa Simba akiwemo huyo Mkude na Ndemla anayetajwa kuja kuichezea Yanga katika msimu ujao wa ligi. Labda nikuweke wazi kuwa sitasajili mchezaji yeyote kutoka Simba,”alisema Zahera.