Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Zuberi Kabwe ameiomba Serikali kuingilia kati dhidi ya baadhi ya vijana wanaokuwa wakijipaka Oil Chafu na kuvamia wanawake na kuwabaka jambo ambalo ni Udhalilishaji wa kijinsia .
Zitto ametoa ombi hilo leo Mei 21,2019 mbungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hoja ya dharura ambapo amesema suala la baadhi ya vijana kujipaka oil chafu na kuvamia wanawake na kuwabaka limekuwa likijitokeza mara kwa mara jimboni kwake ambapo amebainisha kuwa lengo la kujipaka Oil chafu kwa vijana hao ni kurahisisha kuteleza na kutojulikana sura zao pindi wanapokamatwa.
Mhe.Zitto amesema mpaka sasa kuna jumla ya Matukio 43 ya unyanyasaji wa wanawake jimboni kwake tangu Mwaka 2016 na wamekuwa wakipokea vipigo mbalimbali kutoka kwa vijana hao wahuni ,hivyo kuna haja ya serikali kuingilia kati ili kulinda usalama wa wanawake.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi,Kangi Lugola amesema serikali ya Tanzania haiwezi kuvumilia vitendo vya kinyama na udhalilishaji kuendelea katika nchi ya Tanzania hivyo atahakikisha vitendo hivyo vinadhibitiwa
Hata hivyo,Waziri Lugola amesema kuna baadhi ya Taasisi zimekuwa zikifanya uchunguzi na kukuza mambo na kujenga hofu kwa wananchi hata kama ni madogo hali na serikali imeshaanza kuziorodhesha taasisi hizo hali iliyoleta mvutano bungeni kati ya Waziri wa Mambo ya ndani na Zitto Kabwe.
Mwenyekiti wa Bunge Mhe.Nagma Giga amesema suala la ubakaji sio la kuvumiliwa liwe dogo au kubwa hivyo amemwagiza Waziri wa Mambo ya ndani Kangi Lugola kushughulikia jambo hilo.