Wafanyabiashara wa soko la Manzese lililopo Manispaa ya Morogoro wameiomba serikali kuzalisha kwa wingi mifuko mbadala kwani upatikanaji wake kwa sasa ni mdogo huku bei ikizidi kupaa, hali inayopelekea wateja kushindwa kumudu kuinunua.
Wakiongea na www.eatv.tv, wafanyabiashara hao wamesema wamepokea kwa mikono miwili hatua ya serikali kupiga marufuku mifuko ya plastiki kwa lengo la kulinda mazingira lakini changamoto iliyopo sasa ni uhaba wa mifuko mbadala huku wakijikuta wakilazimika kununua mifuko hiyo kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa kwa gharama kubwa.
Shukuru Joramu, ambaye ni mfanyabiashara soko la Manzese Morogoro amesema, "mifuko hii (akiishikika na kuionesha) inauzwa sh 5000 kwa dazani ambapo inakaa 12 na mjini sasa hivi haipo. Naishauri serikali kama viwanda vinavyozalisha hii mifuko viko hapa nchini, basi wasisitize kuongeza uzalishaji".
Mwenyekiti wa wafanyabiashara Soko la Manzese Morogoro, Mengi Jafari amesema kuwa inawawia ugumu namna ya kuwahudumia wateja wao kwani mfuko mmoja unauzwa kwa sh 500 hadi 1000, jambo ambalo wateja wao hawakubali kununua.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt Kebwe Steven amesema hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyeripotiwa kukamtwa kwa kutumia, kuuza au kuzalisha mifuko ya plastiki huku akiwasisitiza Wakuu wa Wilaya kuacha kutumia nguvu kubwa badala yake waelimishe jamii madhara ya mifuko hiyo ya plastiki.