Dar es Salaam. Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Abubakar Zubeir ametangaza kesho Jumatano Juni 5, ni sikukuu ya Eid El Fitri baada ya kuandama kwa mwezi katika mikoa mingi
Akitangaza mwandamo wa mwezi leo usiku akiwa katika Hoteli ya Tanga Beach, Sheikh Zubeir amesema mwezi umeonekana katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Dar es Salam, Arusha, Zanzibar na sehemu nyingine.
“Mwezi umeshuhudiwa na watu waadilifu na mimi nimethibitisha na kesho tujiandae kusherehekea na kuswali Eid El Fitr,” amesema Zubeir
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana Jumatatu Juni 3, 2019 na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Katibu wa kamati ya mwandamo wa mwezi Taifa, Alhad Salum alisema swala ya Idd kitaifa itaswaliwa mkoani Tanga na itaongozwa na Mufti Zubeir.
Alisema Baraza la Eid nalo litafanyikia mkoani humo ambapo mgeni rasmi katika shughuli hizo atakuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Alhad alisema kwa mkoa wa Dar es Salaam swala hiyo itaongozwa na Alhaj Ally Hassan Mwinyi (Rais wa awamu ya pili) na itaswaliwa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.