Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Chama Cha walimu Tanzania (CWT), Clement Mswanyama, amewataka walioshindwa katika chaguzi za uongozi wa nafasi mbalimbali katika Chama hicho kuacha kutoa habari za kupotosha watu.
Hayo ameyasema leo jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kichwa cha habari kilichochapishwa katika gazeti fulani la hapa nchini kilichokuwa kinasomeka “CWT KWAWAKA”.
Mswanyama amesema kuwa katika gazeti hilo waandishi wake walieleza majengo na mali za CWT ,kampuni tanzu ya CWT na TDCL na Benki ya Mwalimu (MCB) kuwa si mali ya walimu jambo ambalo Ni uongo wenye nia ya kuchochea .
Aidha amesema kuwa katiba ya CWT toleo la sita la mwaka 2014 inasema kuwa Mali za chama zitaandikishwa kwa jina la Bodi ya wadhamini pia mikataba yote,hati na dhamana za fedha za chama zote zitamilikiwa kwa jina la Bodi ya wadhamini na kuhifadhiwa kwa katibu mkuu wa CWT.
“Tulizipata taarifa hizo za gazeti kwa masikitiko makubwa na tukajiuliza wenzetu hao wamepata maelezo kutoka kwanani na kwadhamira ipi” amesisitiza Bw.Mswanyama
Hata hivyo amesisitiza kuwa suala hili tunahitaji kuhojiana nao kwa kina na ikibainika wamepotosha umma na walimu kwa ujumla ni lazima tutachukua hatua za kisheria.
Mswanyama amelitaka gazeti hilo kuomba radhi kupitia gazeti lao na Kama wakishindwana watachukua hatua za kisheria juu yao.
Ameendelea kwa kusema, "Ni kweli gazeti hilo lilinukuu ripoti maalum ya mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali(CAG) aliyekagua CWT katika mwaka wa fedha 2016/2017. Mpaka leo tunawahakikishia walimu tumeyafanyia kazi kwa asilimia kubwa na tunaendelea na zoezi hilo kwani ushauri mwingine ulihusu taratibu za kila siku za uendeshaji wa Chama na matumizi ya Mali za fedha za chama".