DC Aeleza Walivyomnasa Mtuhumiwa Kiongozi wa Teleza Anayebaka Wanawake-Kigoma


Serikali ya Wilaya ya Kigoma Mjini imesema kuwa imefanikiwa kumkamata mtu mmoja anayeaminika kuwa kiongozi wa kikundi kinachofanya uhalifu wa kuwabaka na kuwajeruhi wanawake nyakati za usiku, maarufu kama ‘teleza’.

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Kigoma Mjini, Samson Hanga aliwaambia waandishi wa habari kuwa walipata taarifa kuhusu mtuhumiwa huyo aliyemtaja kwa jina la Hussein Hamisi maarufu kama Orosho, na walimfuatilia katika maficho yake.

DC Hanga ameeleza kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya iliunda timu maalum ya jeshi la polisi ambayo ilitengeneza mpango wa kuwatambua na kisha kuwakamata watuhumiwa wote, na kwamba walifanikisha kumkamata Orosho na wenzake tisa.

Akisimulia jinsi walivyomtia nguvuni, alisema jina la mtuhumiwa huyo lilitajwa na wanawake wengi waliowahi kufanyiwa vitendo hivyo pamoja na baadhi ya wananchi.

“Yule kijana alipopata taarifa tunamtafuta alikimbilia kwa mama yake Kijiji cha Kagongo, baadaye akakimbilia tena Kijiji cha Kagunga, juzi jioni tukafanikiwa kumkamata wilayani Kasulu na kuletwa hapa katika kituo cha polisi kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema DC Hanga.

Baadhi ya wanawake ambao ni waathirika wa tukio hilo walisema kuwa wanaishukuru Serikali kwa kufanikisha kuwakamata watuhumiwa wa matukio ya ‘teleza’. Walieleza kuwa teleza walikuwa wakiwajeruhi kwa panga na kisha kuwabaka.

Watu hao walipewa jina la teleza kutokana na namna walivyokuwa wakijipaka oil chafu au mafuta ya mawese ili wanaposhikwa wawe wanateleza.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad