Dkt.Gwajima ameyasema hayo wakati wa kikao cha wadau wa Afya kuwasilisha Taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi kilichofanyika katika Ukumbi wa Takwimu Jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho Dkt. Gwajima amesema huduma Tembezi za Afya ni muhimu kufikishwa katika Ngazi ya Jamii ili wananchi waweze kupata matibabu kutoka kwa madaktari bingwa tena kwa gharama nafuu.
“Huduma hizi zimekuwa zikitolewa na Taasisi tofauti kwa nyakati tofauti na kila Taasisi analenga eneo Fulani ambalo anachagua hivyo kuna maeneo ambayo yamekuwa yakinufaika na huduma hizi mara kwa mara lakini kuna sehemu nyingine hazifikiwi kabisa sasa ni umefika wakati wa kukaa pamoja na kuunganisha nguvu ya wadau wote pamoja na Serikali na kupelekwa huduma hii katika Halmashauri zote ili kila mwananchi mwenye uhitaji anufaike nayo”
Kupitia Kikao hiki cha leo tutaunda Kamati ya Uendeshaji ambayo itahusisha Wataalamu wa OR-TAMISEMI, Wizara ya Afya, Asassi zisizo za Kiserikali pamoja na wadau wanaotekeleza Afua za Afya ambao watakuja na hadidu za rejea zitakazotuongoza katika kutekeleza azima yetu hii kwa ufanisi aliongeza Dkt.Gwajima.
Pia Dkt. Gwajima alisema kuwa “Tunajua tuna vituo vya kutolea huduma vya lakini si wakati wote vituo hivyo vinakuwa na madaktari Bingwa na kwa mwananchi wa kawaidia kusafiri mpaka kukutana na madaktari bingwa ni gharama hivyo tukisogeza huduma hizi tutawatibu wananchi wetu hata yale magonjwa ambayo walikuwa wameyakatia tamaa”Alisema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima aliongeza kuwa Huduma hizi Tembezi zina faida zake kwanza gharama za kuwekeza katika huduma hii ni ndogo lakini inawafikia watu wengi tena kwa muda mfupi.