Majibu ya vipimo hivyo yamethibitisha kuwa Sharon Mitekwa na Melon Lutenyo walizaliwa na mama mmoja, ambaye ni Bi Rosemary Khaveleli.
Matokeo hayo pia yameonesha kuwa msichana Mevis Imbaya aliyekuwa akiishi na Melon kama pacha mwenzake, si dada yao halisi, na Bi Angeline Omina, aliyekuwa akiishi na Sharon kama mama yake mzazi katika mtaa wa Kangemi, Kaunti ya Nairobi ndiye mama mzazi wa Mevis.
Uchunguzi huo uliendeshwa na Dkt Ahmed Kalebi kutoka maabara ya Lancet, juu ya mapacha ambao walitenganishwa katika hali tatanishi mnamo 1999, mara tu baada ya kuzaliwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kakamega, na kuonesha kuwa chembechembe zao za DNA zinalingana kwa asilimia 100, hali inayothibitisha kuwa ni pacha halisi.
Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza mnamo Aprili kupitia mtandao wa Facebook miaka 19 baada ya kuishi katika makazi na maisha tofauti, baada ya pacha mmoja kuona mtu aliyefanana naye kwa kila kitu na kuamua kumuomba urafiki, na ndipo alipobaini kuwa anafanana na si kwa bahati mbaya bali kuna kitu zaidi na kuanza kufuatilia, ndipo ikagundulika walizaliwa siku moja na hospitali moja.
Walijikuta wakilelewa na mama tofauti, jamboa mbalo mpaka sasa halijajulikana kilichotokea mpaka watoto hao kubadilishiwa wazazi, na kulelewa na watu ambao si wazazi halisi.