DONALD Trump Afyata MKIA..Aaeleza Sababu ya Kusitisha Ghafla Amri ya Kuishambulia Iran


Rais wa Marekani, Donald Trump ameeleza sababu ya kuamua kusitisha amri yake ya kuishambulia rasmi Iran kutokana na kutunguliwa kwa ndege ya jeshi la nchi hiyo isiyo na rubani.

Akizungumza jana na NBC, Rais Trump alisema kuwa vikosi vya nchi hiyo vilikuwa tayari kuanza kufanya mashambulizi dhidi ya Iran kwa lengo la kujibu hatua za kutunguliwa kwa ndege yake, lakini alishusha pumzi kwa sekunde moja na kufikiria kuhusu idadi ya wananchi 150 wa Iran ambao wangepoteza maisha.

“Nilifikiria kuhusu hilo kwa sekunde moja na nikasema, ‘unajua nini, wametungua ndege ambayo haina rubani, lakini hapa tutakaa na miili 150 ya watu ambao wangekufa kama mashambulizi hayo yangefanyika angalau kwa nusu saa baada ya kutoa idhini,” alisema Trump.

Alisema kuwa Iran inaweza kukutana na adhabu ya kutokomezwa na itaendelea kukabiliwa na vikwazo vingi vya kiuchumi endapo itakaidi makubaliano kuhusu silaha za kinyuklia.

Hata hivyo, alisema kuwa bado kuna nafasi ya kufanya mazungumzo na Iran kuhusu makubaliano ya nyukilia lakini kama watakaidi wataendelea kukumbwa na vikwazo hivyo.

Nayo Iran imesema kuwa iliitungua ndege ya Marekani kwa sababu iliingia kwenye anga lake na ilikuwa na nia ya kufanya ujasusi. Imesema kuwa itawasilisha malalamiko yake kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na uvunjifu wa sheria za Kimataifa. Marekani nayo imeeleza kuwa itaitisha Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu ili kuijadili Iran.

Marekani imeendelea kusisitiza kuwa ndege yake ilikuwa katika anga la kimataifa na haikugusa anga la Iran.

Iran kupitia televisheni ya taifa, ikionesha mabaki ya ndege ya Marekani iliyotunguliwa, imeeleza kuwa ingawa haihitaji kuingia vitani itaendelea kulinda anga na ardhi yake dhidi ya adui yeyote.

Kwa upande mwingine, Serikali ya Urusi imeonya kuwa mgogoro kati ya mataifa hayo ni hatari endapo yataingia vitani kwani itasababisha madhara makubwa kwa sehemu kubwa ya dunia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad