Rais John Magufuli, Disemba 2015 aliunda Baraza lake la kwanza la Mawaziri alilolitangaza kwa awamu mbili likiwa na mawaziri 19 katika wizara 18 wakati huo.
Akitangaza baraza hilo kwa mara ya kwanza, Desemba 10, mwaka huo, Rais Magufuli hakutaja majina ya mawaziri wanne, nafasi ambazo alizijaza wiki mbili baadaye, Desemba 23.
Tangu uteuzi huo ulipokamilika hadi sasa, wengi miongoni mwa mawaziri hao ama wameondolewa katika nafasi zao au kuhamishwa kutokana na sababu mbalimbali.
Hata hivyo, katika orodha ya mawaziri hao waliotajwa mwaka 2015, wapo saba wanaoendelea kuhudumu kwenye nafasi zao mpaka sasa.
Hao ni William Lukuvi (Ardhi na Maendeleo ya Makazi), Dk Hussein Mwinyi (Ulinzi), Ummy Mwalimu (Afya), Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Dk Philip Mpango (Fedha na Mipango), January Makamba (Muungano na Mazingira) na Jenista Mhagama (Sera, Uratibu na Bunge).
Hadi sasa, Rais Magufuli amewaondoa mawaziri 10 na manaibu wanne, akiwapandisha vyeo manaibu watano na kuwabadilishia wizara mawaziri wanne.
Aliowapandisha ni Selemani Jafo aliyekuwa naibu waziri wa Tamisemi. Isack Kamwelwe aliyekuwa naibu waziri wa maji na umwagiliaji ambaye alipandishwa kuwa waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.
Kwenye orodha hiyo, pia yupo Dk Hamis Kigwangalla aliyeanza kama naibu waziri wa afya kabla ya kupandishwa kuwa waziri wa maliasili na utalii.
Pia yumo Luhaga Mpina aliyekuwa naibu waziri wa muungano na mazingira na sasa ni waziri wa mifugo na uvuvi na Dk Medard Kalemani aliyekuwa naibu waziri wa nishati na madini sasa ni waziri wa nishati.
Pamoja na sababu nyingine, kupanda kwa manaibu hao kumechangiwa na kuongezeka kwa wizara. Katika kipindi hicho, Rais Magufuli aliongeza wizara ya uwekezaji ambayo ilikuwa kwenye viwanda, biashara na uwekezaji.
Pia aliivunja iliyokuwa wizara ya nishati na madini na kuunda mbili.
Vilevile, amefanya hivyo kwa iliyokuwa wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi kupata wizara ya kilimo na wizara ya mifugo na uvuvi.
Alipoulizwa siri ya kuendelea kubaki kuihudumia Wizara ya Elimu hadi leo tangu alipoteuliwa, Profesa Ndalichako alisema hilo ni swali gumu kwake kwani mwenye majibu sahihi ni aliyemteua.
“Kwa wenzetu wanaotenguliwa naamini ni changamoto za kazi ndizo zinasababisha hilo,” alisema Profesa Ndalichako.
Hata Waziri Makamba alisema Rais Magufuli ndiye mwenye siri ya yeye na wenzake kuendelea kudumu katikanafasi zao kwenye Baraza la Mawaziri.
“Kwa mujibu wa utaratibu, Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuteua, kutengeua au kumbadilisha waziri,” alisema mbunge huyo wa Bumbuli.
Kwenye orodha ya mawaziri waliobadilishiwa wizara yumo Profesa Makame Mbarawa aliyeanzia wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano kisha kupelekwa maji na umwagiliaji. Mwingine ni Profesa Palamagamba Kabudi aliyekuwa waziri wa sheria ambaye amebadilishana na Dk Augustine Mahiga aliyenza na wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.
Pia, Dk Harrison Mwakyembe alianzia katiba na sheria kabla ya kuhamishiwa habari, michezo, sanaa na utamaduni.