Hotuba ya Upinzani Wizara ya Fedha yakatazwa kusomwa Bungeni

Spika wa Bunge, Job Ndugai amekataza kusomwa kwa hotuba ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kuhusu bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2019/20 akisema imejaa lugha za kuudhi.

Ndugai alitoa uamuzi huo jana bungeni mara baada ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti, Mashimba Ndaki kuwasilisha maoni ya kamati hiyo.

Baada ya maoni ya kamati kusomwa, Spika Ndugai alisimama na kusema kambi rasmi ya upinzani haitawasilisha taarifa yake kutokana na kuwa na makosa mengi, zikiwemo lugha za kuudhi.

“Haitakuwa hivyo kwa sababu ya makosa yao, sijui kama kuna haja mtaona jinsi ilivyo, sijui kwanini wanafanya hivyo, mkiacha huko ndani lugha mnazotumia ni masikitiko makubwa.

“Vitabu hivi vinakaa muda mrefu, wanakuja vitukuu vyete kufanya ‘reference’ (marejeo), huu ni ushauri wa bure tu. Haiwezekani Bunge limekuweka pembeni halafu wewe unapitisha kwa mlango wa nyuma,” alisema Ndugai, akimlenga Halima Mdee, ambaye amesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge.

Mbunge huyo wa Kawe, jina lake lilikuwa kwenye moja ya kurasa za hotuba hiyo iliyokataliwa.

Mdee amesimamishwa na Bunge kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge kuanzia huu unaoendelea wa 15 wa Bunge la Bajeti kwa kosa la kuunga mkono kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kwamba Bunge ni dhaifu.

Hotuba hiyo iliyozuiwa ilikuwa isomwe na Mbunge wa Momba, David Silinde  (Chadema) ambaye ni Naibu Waziri kivuli katika Wizara ya Fedha na ndiye aliyesoma hotuba hizo kwa miaka miwili kutokana na Mdee kuwa nje kwa adhabu mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad