Inasikitisha! Mume na Mke Wauawa kwa Kuchinjwa Shingoni Kisa Shamba

WAKAZI wa Kijiji cha Masengwa wilayani Shinyanga, Manyara Ndelema (48) na mkewe Nyamizi Mserengeti (40), wameuawa kwa kuchinjwa shingoni kwa madai ya kuwapo migogoro ya mashamba ya kifamilia.



Inadaiwa kuwa Ndelema alinunua mashamba ya familia yao baada ya kuuziwa na wanafamilia ili wapate kumaliza matatizo yaliyokuwa yakiwaandama, lakini baada ya ndugu zake hao kukosa mahali pa kulima, waliibua mgogoro kuyataka mashamba hayo na kusababisha mauaji yake pamoja na mkewe.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Richard Abwao, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea Juni Mosi, mwaka huu, majira ya saa 7:00 usiku.

Alisema Ndelema akiwa amelala na mkewe, walivamiwa na watu na kisha kukatwa maeneo ya miili yao ikiwamo shingo na mabega.

Alisema baada ya mauaji hayo, wahusika walikimbia kusikojulikana na Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali na kuwakamata wawili na baadaye kuwakamata watuhumiwa wengine wanne juzi Nzega mkoani Tabora.

“Chanzo cha mauaji ya watu hawa mume na mke ni ugomvi wa mashamba ya kifamilia, ambayo waliyanunua kutoka kwa ndugu zao waliokuwa wakikabiliwa na shida mbalimbali. Baada ya kuyanunua ndugu hao walianza kuyataka kwa nguvu baada ya kukosa maeneo ya kulima, hivyo kuamua kuwaua ili wapate kuyamiliki tena,” alisema Abwao.

“Miili ya marehemu tumeikabidhi kwa ndugu zao wengine kwa ajili ya taratibu za mazishi baada ya daktari wa serikali kumaliza kuifanyia uchunguzi, ili wapate kupumzishwa kwenye makao yao ya milele,” aliongeza.

Aidha, alisema watuhumiwa hao sita baada ya taratibu za kiupelelezi kukamilika, watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad