Iran Yasema Mashambulizi ya Kimtandao Yaliyofanywa na Marekani Dhidi Yake Yamefeli na Hayajaleta Madhara Yoyote


Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa mashambulizi ya hivi karibuni ya kompyuta ya Marekani dhidi ya mfumo wa makombora wa Iran yameshindwa kuleta madhara na kwamba mwaka jana pekee Tehran ilifanikiwa kuvunja makumi ya mamilioni ya mashambulizi ya kompyuta dhidi yake.

Waziri wa Habari na Teknolojia ya Mawasiliano wa Iran, Bw. Mohammad Javad Azari Jahromi ameandika leo Jumatatu katika mtandao wake wa Twitter kwamba vyombo vya habari vimeuliza iwapo mashambulizi ya kompyuta yanayodaiwa kufanywa na Marekani dhidi ya Iran yamefanyika au la?

"(Napenda kujibu kwamba) wamejaribu sana lakini hadi hivi sasa hakuna shambulio lao lolote lililofanikiwa." Amesema

Siku ya Alkhamisi, vyombo vya habari vya Marekani vilidai kuwa nchi hiyo imeshambulia mifumo ya kompyuta inayoendesha maroketi na makombora ya Iran.

Mashambulizi hayo ya kompyuta ya Marekani yalianza mara baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kutungua ndege kubwa na ya kisasa kabisa ya kijasusi ya Marekani ya RQ-4A global Hawk, iliyoingia katika anga ya Iran kinyume cha sheria.

Mfumo wa kujilinda na mashambulizi ya anga wa Khordad 3 wa Iran ndio uliotungua ndege hiyo ya Marekani katika anga ya Ghuba ya Uajemi, kusini mwa Iran.

Waziri huyo amesema kuwa; "kwa muda mrefu sana tumekuwa tukikabiliana na ugaidi wa mashambulizi ya kompyuta kutoka kwa adui… mwaka jana tulifelisha mashambulizi milioni 33 kwa kutumia mfumo wetu maalumu wa kitaifa wa kujilinda na mashambulizi ya kompyuta."
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad