Rais Magufuli ametaja sababu za kumng’oa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere, huku akitoa pole kwa walioteuliwa kushika nyadhifa hizo.
Rais Magufuli alitaja sababu hizo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni ambao ni Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, Kamishna Mkuu wa TRA, Edwin Mhede na Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Kichere.
Katika mkutano huo, Rais Magufuli alishuhudia Kampuni ya Bharti Airtel ikiikabidhi serikali gawio la Sh. bilioni tatu la miezi mitatu kuanzia Aprili pamoja na fedha binafsi iliyotolewa na mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo, Sunil Mittal, dola za kimarekani milioni moja (Sh. bilioni 2.2).
Akitaja sababu za kuwaondoa kwenye nafasi zao Kakunda na Kichere, Rais Magufuli alisema: “Tutaambizana maneno mazuri mazuri, lakini maneno mazuri hayasaidii, ukitaka maneno mazuri kaelezwe na mume wako, mke wako basi, lakini sisi tunataka matokeo mazuri basi,” alisema.
Rais Magufuli alisema jukumu lake ni kuteua ili kusudi nia ya Watanzania wanayohitaji ikatimie.
“Ninapotengua mahali siyo kwamba wewe ninakuchukia, nakupenda tu na ninakupongeza mheshimiwa Joseph Kakunda kwa kuja, huku ndiko kukomaa kisiasa, hizi kazi ni muda mfupi, maisha yenyewe ni ya muda mfupi, hakuna kazi ya kudumu,” alisema.
Alisema, “Lakini amejitoa amekuja, safi sana lakini ni ukweli kwenye wizara hakuisukuma ninavyotaka, ni mimi ninataka matokeo na Watanzania walionichagua wakatupigia kura wanataka kuona utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.”
“Changamoto za wafanyabiashara kwani kulikuwa na ubaya gani, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Waziri mwenyewe siwangekuwa wameshapanga mikutano wa wafanyabiashara, palikuwa na dhambi gani? Nani angewakataza? kwamba leo tunazungumza na wafanyabiashara wa Kanda ya Ziwa, leo Kanda ya Kaskazini, leo Kusini, nisikie shida na changamoto zao.”
Rais Magufuli alisema: “Wanasema hawajawahi kumuona, hata ningeuliza hata Manyanya (Stella Manyanya, Naibu Waziri wa Viwanda) nikasema labda hawajawahi kumuona, kwa sababu Watanzania siyo wanafiki,” alisema.
Kuhusu korosho, Rais Magufuli alisema wamefanya biashara hiyo zaidi ya tani 223,000 na kuhoji ni tani ngapi zimeshauzwa.
“Wizara inaitwa Wizara ya Viwanda na Biashara ni biashara gani inafanya? Wizara ya Kilimo imetimiza wajibu wake, imenunua, wanajeshi wametimiza wajibu wao wamesomba korosho yote wameweka kwenye maghala, Wizara ya Biashara inafanya nini? Ipo tu, korosho zimekaa,” alihoji.
“Wakati huo Tanzania ilikuwa ndiyo wazalishaji peke yetu, tumesubiri hadi mwezi wa tatu mpaka wa nne ukaingia nchi nyingine za Benin, Nigeria, Cote d’Ivoire nazo zikazalisha bado hatujauza, wapo tu, sasa unakuwa unajiuliza wa nini? Kupeperusha bendera barabarani? Haiwezekani,” alisema.
Rais Magufuli alimwambia Bashungwa kuwa inawezekana wamempongeza, lakini alifikiri wangempa pole kwa sababu akiona mambo hayaendi atamtengua.
“Kwa sababu nitaangalia yale ambayo hayaendi, nikiona hayaendi ninatengua nasema ukweli, Prof. Palamagamba Kabudi (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, wamezungumza tu hapa hawataki kusema, lakini kama ni ‘pumbavu’ kwenye simu wametukanwa mno waulizeni,” alisema na kuongeza:
“Wananizidi umri, lakini neno pumbavu linakuja tu haraka haraka, ndiyo ukweli kwa sababu hii kazi siyo ya kubembelezana, lazima tuipeleke kijeshi, mwanajeshi usiposonga mbele kupigwa risasi na mwenzako siyo tatizo, mpo kwenye vita… hatuwezi kukawa na vita halafu tukawa tunabembelezana na kupeana maneno mazuri tu, lazima tubadilike, wanaotuangalia hawana muda wa kusubiri.”
Rais Magufuli alisema Wizara ya Viwanda na Biashara wamebangua tani 2000, nyingine wanasubiri atelemke nani ndiyo waziuze.
“Na una waziri pale wa biashara ana vyombo vyote vya kufanya biashara nikitakiwa nimpandie kutoka juu mpaka chini, pamoja na wewe Muhende ulikuwa uende huko huko, ukienda kafanye kazi usibembeleze mtu usimchekee mtu nafuu wakuchukue mimi ninayekuteua nikusimamie kinyume na hapo utakwenda kunusa tu pale urudi Karagwe,” alimweleza waziri mpya.
Rais Magufuli alimtaka waziri huyo yale ambayo yamekaa yatatuliwe, viwanda vilivyoshindwa kuendelezwa visiorodheshwe tu, vitafutiwe watu wavichukue.
“Kiwanda kama cha Mbeya cha nguo kinakwenda kubadilishwa kiwe cha pipi, hakiwezekani, tunaonekana tunakula pipi tu, zipo changamoto nyingi kashirikiane na wenzako kuzitatua,” alisema.
Akigeukia kilichomwondoa Kichere, Rais Magufuli alisema Waziri Mpango amezungumza alivyokuwa pale Kamishna wa TRA, aliipandisha kutoka Sh. bilioni 850 hadi trilioni 1.3.
“Nikampandisha cheo kutoka TRA akawa Waziri wa Fedha, sasa wengine mnaokwenda mnasimamia hapo hapo kana kwamba ni fomula, lakini tatizo malalamiko ni mengi na hamchukui hatua, kama kuna ujumbe mfupi nimekutumia kamishna uliyeondoka yawekezana zinazidi 20 au 30 zingine nilikuwa natuma saa nane za usiku, nyingine saa tisa na nyingine saa kumi kwa sababu watu wanapolalamika ninamtumia na jamaa huyu ni kama diplomat (mwanadiplomasia) anasema nimepoka mheshimiwa,”
Aliongeza, “Ukifuatilia hakuna matokeo, ndiyo ukweli, mimi huwa sisahau ndiyo dhambi niliyonayo, haiwezekani mkurugenzi wako wa kukadiria anatoa makadirio ya kijinga kwa wafanyabiashara upo unamwangalia tu wakati una nguvu unashindwa kuitumia, unaona makusanyo ya kodi ya ndani yanashuka, labda huyu wa sasa imepanda kidogo, lakini hakuna hatua inayochukuliwa.”
Rais alisema: “Unaona kuna wafanyabiashara wanapakia mizigo wanaiandika inakwenda Tunduma hadi nchi jirani, wakifika Tunduma wanagongewa mihuri wanarudi kuishusha wakati barabara yote TRA, lori linatembea kilometa 1,300 linasema linakwenda nchi jirani wanachukua nyaraka wanagonga mpakani wanarudi, kama gharama mtu ameamua kusafirisha hadi Tunduma anarudi halafu amehonga za kugonga muhuri, zingejumlishwa zote angetelemsha mizigo yake hapa si mngemsaidia atumie mafuta vizuri.
Rais Magufuli alibainisha kuwa kuna mwekezaji alikuja na vifaa vyake anataka kuchimba dhahabu, lakini vimekaa zaidi ya mwaka alikuwa kiasi kidogo akaongezewa zaidi.
“Badala ya kuangalia huyu atawekeza hiki atatoa ajira na serikali itapata mapato kutoka kwenye dhahabu, utafikiri TRA wote hawakusoma, ndiyo maana nikasema siwezi, ndio maana siku ile walivyokusema nakuuliza unasema hujui unamwangalia mtu wa nyuma yako utamwangalia mpaka lini ukikuta hawapo, nafuu utoke na wewe hapo hapo,” alisema.
Rais Magufuli alimwambia Kichere kuwa amempeleka Njombe akajaribu ukatibu tawala na endapo akiusimamia vibaya atamtoa.
Aliwambia kuwa kuna watu wamebobea pale TRA na kumtaka akawakamate ili kodi ipatikane.
“Hakuna nchi duniani iliyoendelea bila kodi, niache kuwalipa mishahara si nitawakuta Ikulu wamesimama, usicheke na mtu, ni sawa na useme usiende mbinguni tutakuombea wote tunaofaidi utakwenda kwa nguvu tutakusukumiza Watanzania wote milioni 55 uingie mbinguni,” alisema.
Pia alimtaka akashirikiane na wafanyabiashara ili wampe taarifa nyingi na wale walioghushi siku za nyuma kutokana na mazingira akakae nao waseme wanaweza kulipa kiasi gani, kwa sababu anayo mamlaka ya kusamehe asilimia fulani.
Kuhusu watumishi wanaokwenda kwa wafanyabiashara kuwapa makadirio makubwa na kusema wametumwa juu, amemtaka asiogope kuwafukuza, awashike na kuwapeleka mahakamani.
“Kama unawafanyakazi 1000, halafu 200 wakaishia kufukuzwa na kwenda mahakamani sawa tu, lakini ukiwa mtaratibu watakukaribisha na siku ukiingia ofisini watakuletea au karibu wote watakuita bosi hata kama naye ni bosi achana na sherehe, jana nimekutumia ujumbe wa mtu analalamika, kabla sijakuapisha,” alisema.
Alisema kuna makamishna wa TRA katika mipaka, ambapo mpaka wa Rusumu unafanya vizuri lakini Tunduma na Sirari hakufai.
JPM Aanika Sababu za Kumtumbua Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
0
June 11, 2019
Tags