Kamwelwe atoa agizo kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA)

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaac Kamwelwe, ameiagiza Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kukutana na madereva teksi, wahudumu wa hoteli na waongoza utalii ili kuongeza ufanisi wa sekta ya usafiri wa anga nchini.

Akizungumza katika kongamano la pili la wadau wa sekta ya usafiri wa anga Dar es Salaam , Kamwelwe alisema watoa huduma hao ni watu muhimu katika shughuli za utalii na usafiri wa anga, kwa sababu wana mawasiliano ya watalii wengi ambao wamewahi kutembelea nchini.

 “Hamza (Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari) nendeni Arusha, Kilimanjaro na Mbeya mkutane na ‘taxi drivers’, ‘tour guiders’ na wahudumu wa hoteli, mtapata mambo ya ajabu, mnaweza kukuta kijana ana namba 200 za watalii.

“Watalii ni watu wasiopenda kutumia muda mwingi safarini na sisi hivi karibuni tunakuwa na ndege za moja kwa moja,” alisema Kamwelwe.

Alisema wizara yake iko kwenye hatua za mwisho za mazungumzo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ili ianze kutoa mikopo kwa wanafunzi wa fani za urubani na uhandisi wa ndege kuwezesha kuandaa wataalamu wa ndani.

Aidha alilitaka Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuongeza safari moja ya ndege kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam itakayokuwa ikitoa huduma mchana tofauti na sasa ambapo kuna safari tatu wakati wa asubuhi na jioni.

Aliongeza kuwa huenda kuanzia Julai shirika hilo likaanzisha safari ya kutoka Mwanza kwenda barani Ulaya na kufungua fursa kwa wafanyabiashara kutumia soko la samaki lililopo nchini humo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad