Vijana 6 Mkoani Njombe wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kugushi vyeti katika zoezi la usahili wa kujiunga nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
Hayo yamesemwa Jana Juni 29 na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Olesendeka alipokutana na waandishi wa habari Mkoani humo ambapo amebainisha kuwa, hatua hiyo ni maamuzi ya wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ambao wamekubaliana, kutengua Mchakato mzima wa zoezi hilo ili kuanza upya kwa kuzingatia misingi ya Sheria na Haki.
Olesendeka amesema, kutokana na vitendo vya udanganyifu ikiwemo kugushi uraia, wajumbe wakamati hiyo wametengua uteuzi wa nafasi za vijana waliotarajiwa kujiunga na Jeshi hilo kwa ajili ya Mafunzo.
“Baada ya kupitia wilaya moja baada ya nyingine, tumebaini kuwepo kwa udanganyifu wa vyeti kwa ikiwemo vyeti vya kuzakiwa, vyeti vya elimu ya msingi, na hata kuwepo ya viashiria kwamba, wengine Uraia wao una mashaka,” alisema Olesendeka.
Alisema wamelazimika kufanya maamuzi ya kutengua uteuzi wa vijana hao nakusitisha zoezi zima la uteuzi wa vijana wanaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa.
Amesema, wametangaza vijana hao wapeleke maombi upya na ameongeza kua, watu wote waliotajwa na kuhusika na udanganyifu kwa sasa wanaendelea kuhojiwa na Vyombo vya ulinzi na usalama.
Ameongeza kuwa, kwa sasa watu ambao wako chini ya ulinzi ni vijana sita na kubainisha kuwa wamechukua hatua zote hizo ili kutoa haki kwa watoto wa wakulima, watoto wa wavuvi, wafugaji na watoto wa maskini wa nchi hii ili nao waweze kujiunga na Jeshi la kujenga Taifa JKT ambayo ni haki yao.
Kama ulipitwa
Wiki mbili zilizopia, Mikoa yote nchini imeendesha zoezi la kupokea maombi ya vijana watakaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa katika ngazi za wilaya na baadae kufanyiwa usaili katika ngazi za mikoa ili kupata vijana wanaostahili.