Kodi zinaua biashara Kariakoo - Wabunge

Wabunge wameitaka serikali ije na mkakati wa kurejesha biashara ya kimataifa katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Wamesema biashara Kariakoo inakufa kwa sababu ya utitiri wa kodi na kwamba wafanyabiashara wamekimbilia nchini Uganda.

Hoja hizo zilitolewa na wabunge hao wakati wakichangia mjadala wa bajeti ya serikali na hali ya uchumi, iliyowasilishwa mwishoni mwa wiki bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Wabunge wamesema serikali ina haja ya kufanya jambo la mkakati kurudisha biashara katika soko la Kariakoo.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) alisema Waziri wa Fedha amempa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kadirio la kukusanya Sh trilioni 1.7 na kwamba akishindwa atamtumbua.

"Nasema haya in a very good faith, Kamishna akishindwa kutimiza hayo anaweza kutumbuliwa, sasa bado kuna shida kwenye masuala ya kodi na sheria zetu, Mheshimiwa Spika ili tukusanye kodi lazima tuzalishe na ili tuzalishe vikwazo vya kodi viondolewe"alisema Bashe.

Bashe aliongeza kuwa sheria za kodi nchini zinapaswa kufanyiwa marekebisho kama vile kodi ya mapato, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na nyingine ili kufikia malengo na kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya kazi zao kwenye mazingira tulivu.

Aidha, alisema ili nchi ikusanye kodi, ni lazima ifanye biashara na sekta ya kupewa kipaumbele ni sekta ya kilimo, ambayo takwimu zinaonesha kuanzia mwaka 2016 mpaka 2018/19, uwekezaji mikopo umeshuka kutoka asilimia 11 mpaka -4.

"Sasa mtaona biashara zinashuka na kama hatutafanya jambo hatutaweza kutoka kibiashara hapa, nikuombe Waziri Mpango na najua hii utakumbana na matatizo serikalini, fanya maamuzi yafuatayo; muite Waziri wa Viwanda na Biashara, kaa naye muombe mfanye mabadiliko makubwa, tuna sheria hapa, tuna sheria ya Camatec, tuna sheria ya TIRDO, tuna sheria ya EPZA, tuna sheria ya Tantrade, haya mataasisi yanajichanganya yenyewe, hebu fanyeni jambo kuweka mambo sawa,"alishauri Bashe.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Mvomero, Said Murad (CCM)alisema makadirio ya kodi yasiyo sahihi kwa wafanyabiashara ni chanzo cha kufa kwa soko la Kariakoo.

Alisema hiyo imewafanya wafanyabiashara kutoka nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Zambia, Uganda na Zimbabwe, sasa kulikimbia soko hilo na kwenda nchini Uganda.

Murad alisema tatizo lililopo ni ukadirio usio sahihi wa kodi unaofanywa na TRA pamoja na kutokuruhusu wafanyabiashara wanaonunua bidhaa China na Dubai kwenda na fedha taslimu.

"Biashara za Dubai na China zimetawaliwa kwa kulipa fedha taslimu. Ni muhimu kwa Benki Kuu (BoT), ueleze utaratibu wa kupeleka fedha taslimu ukoje. BoT wasaidie kuhakikisha biashara inarudi Kariakoo, kwa sasa imepotea katika ramani ya biashara.

Aliongeza "Tulikuwa na Kariakoo ya wafanyabiashara kutoka Malawi, Burundi, Congo, Uganda na Rwanda, BoT na TRA lazima wajiulize kuna nini na sababu zipi tulizopoteza biashara Kariakoo."

Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara, alisema kamati hiyo ilimshauri Rais John Magufuli, kukutana na wadau wa biashara kuzungumza nao, jambo ambalo amelifanya.

"Wanaozungumza maneno ya pembeni wameishiwa hoja, mwenyekiti wa kamati ya viwanda ndio mimi. Naujua ukweli. Tozo kero 54 zimeondolewa sio jambo dogo, ni jambo kubwa linalopaswa kupongezwa," alisisitiza.

Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, alisema wafanyabiashara hususan wadogo, wanakabiliwa na tatizo kwenye mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD).

"Mashine za EFD zimekuwa kero, sijajua tatizo ni kampuni zilizopewa tenda au la. Kila siku ni mbovu, sasa zimekuwa mtaji kwa watu, utaambiwa mashine mbovu nunua nyingine," alibainisha.

Kadhalika, alisema kwenye biashara ya usafirishaji hususani malori, kunatakiwa kufanyike uchunguzi kubaini sababu za wafanyabiashara hao kusajili malori nje ya nchi.

"Bandari inafanya vizuri lakini usafirishaji wanafaidika Burundi, Rwanda na Uganda ambapo magari yote ya Tanzania yanasajiliwa kwenye nchi hizo na ushahidi zipo gari zinakuja zitasajiliwa Rwanda,"alisema.

Alisema"Gari zote za usafirishaji tatizo ni nini?. Tujiulize kuna shida gani, jaribuni kukaa na wafanyabiashara kubaini kuna tatizo gani."

Kwa upande wake, Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuph Salim Hussein, alisema katika eneo la Kariakoo zaidi ya hoteli 50 zimefungwa, wabeba mizigo wanakosa ajira na wafanyabiashara wanafunga biashara zao.

"Juzi kuna kampuni ya simu imempatia Rais Magufuli gawio la shilingi bilioni tatu, hebu tuangalie kama viwanda vikifanya hivyo, kampuni zikifanya hivyo, serikali itapata kiasi gani cha fedha? Mfumo huo ndio ambao Sweden inavyofanya kazi, serikali yao imeweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara," alibainisha.

Salim alisema mwaka jana alichangia hoja bungeni, akisema kodi ya milioni 40 kwa kontena inayotozwa bandarini, itaua biashara, kwani wafanyabiashara wanaleta makontena wakidai ya nje ya nchi kisha wanalipa milioni 10, lakini yakifika Uganda, nguo zinarudi Tanzania.

"Rais amekutana na wafanyabiashara wakaeleza yale yale. Mlituletea mtaalamu wa biashara hapa bungeni kutupa semina, lakini tulipomuuliza maswali alikuwa anakwepa, hawa wataalamu wetu wajitathimini," alisema Salim.

Mbunge wa Ukerewe (CCM), Joseph Mukundi, alisema uchumi unaonesha kupanda kwa asilimia saba, ambazo zilizotokana na sekta mbalimbali za uchumi zilizofanya vizuri ikiwemo sekta ya kilimo ambayo imekua kwa asilimia 5.3.

Awali akichangia mjadala huo, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) alisema uamuzi wa kufuta tozo 54 utasaidia kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini, lakini bado kuna tozo nyingine zinapaswa kuangaliwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad