TAMASHA kubwa la kuchangisha fedha lililopewa jina la ‘Kubwa Kuliko’ limepangwa kufanyika leo huku waratibu wake wakitamba litakuwa ni ‘bab kubwa’ na nchi nzima itatetema kwa saa sita.
Tamasha hilo limepangwa kufanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Upanga jijini Dar es Salaam kuanzia saa nne kamili asubuhi na kumalizika saa kumi kamili jioni. Katika tamasha hilo litakaloweka historia, viongozi wa Yanga wanatarajia kukusanya Shilingi Bilioni 1.5 zitakazotumika katika usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Katibu Mkuu wa Kamati hiyo ya Uhamishaji ya Yanga, Deo Muta alisema maandalizi ya tamasha hilo yanakwenda vizuri na inasubiriwa siku yenyewe husika.
Muta alisema, katika tamasha hilo wanatarajiwa kuwepo viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, viongozi wa dini Josephat Gwajima na Zachary Kakobe.
Aliongeza kuwa, watakuwepo wasanii mbalimbali akiwemo Harmonize, Juma Nature, Steve Nyerere, Wolper, Mzee Bwaxy pamoja na wachezaji wa zamani wa Yanga waliocheza kwa mafanikio makubwa.
“Maandalizi ya tamasha hilo la Kubwa Kuliko yamekamilika na kinachosubiriwa ni siku yenyewe pekee vitu vingi tumevimeandaa vizuri na tiketi zitauzwa kwa viwango tofauti ambavyo vitakuwa VVIP meza ya watu 10 Shilingi Milioni 10.
“VIP meza ya watu 10 Shilingi Milioni Tano, VIM 1 meza ya watu 10 Milioni Moja, VIM 2 kwa mtu mmoja Shilingi 100, 000 na kawaida itakuwa Shilingi 50,000. “Tutaitetemesha nchi siku ya Jumamosi katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, sidhani kama kuna Mwanayanga yeyote ambaye atashindwa kuhudhuria. Lengo letu ni kukusanya Bilioni 1.5,” alisema Muta.
Leo ndo Leo Yanga na Tamasha Lao la 'Kubwa Kuliko' Kikwete, Majaliwa Ndani
0
June 15, 2019
Tags