MAKALA YA MALOTO: Paul Makonda ni Mjanja, Tajiri au Mkarimu zaidi
0
June 26, 2019
By Luqman Maloto
Naomba nichambue maneno matatu ya Kiingereza; “Go-Taker”, “Go-Getter” na “Go-Giver”. Go-Taker humpambanua mwenye malengo ya kufanya kitu ili apate anachokusudia. Go-Getter ni yule analenga kufanikisha matokeo ya kila upande. Go-Giver ni mkarimu, anayelenga kutoa kuliko kupata.
Go-Taker Leader ni kiongozi mchukuaji. Go-Getter Leader ni kiongozi mfanikishaji. Na Go-Giver ni kiongozi mtoaji (mkarimu).
Namuona Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa ni kiongozi mtoaji kuliko wakuu wote wa mikoa.
Kuna wakuu wa mikoa wafanikishaji. Nami ni mfuasi wa viongozi wenye kufanikisha kuliko watoaji. Wafanikishaji hutengeneza matokeo makubwa kwa jamii wanayoiongoza, wakati watoaji huwatendea ukarimu wale wanaoguswa na misaada.
Kiongozi mfanikishaji ni yule ambaye huyatazama matatizo ya kijamii na kuyatatua. Mathalan, watu wanateseka kwa sababu hawana uwezo wa kumudu matibabu, hivyo anatengeneza mpango wa kiserikali wa bima ya afya kwa kila kaya. Kiongozi mtoaji atampa fedha za matibabu mgonjwa aliyemwona, ambao hajawaona wataendelea kupigika.
Wapo wakuu wa mikoa wafanikishaji. Pongezi kwao. Lakini pia wapo watoaji, na kati yao simwoni, ambaye anamfikia au kumkaribia Makonda.
Makonda alienda Simba na kutoa Sh20 milioni, Sh10 milioni kwa golikipa Aishi Manula na Sh10 milioni nyingine kwa wachezaji wengine wa timu hiyo ambao walishinda tuzo mbalimbali. Akaenda Yanga na kutoa eneo kubwa Kigamboni kwa ajili ya timu hiyo kujenga uwanja wa mpira.
Aliwajibu polisi Dar es Salaam kuwa hawezi kuwapa gari la thamani ya Toyota IST kwa sababu halina hadhi. Akasema polisi anawanunulia gari lenye hadhi. Kwa maana kwamba lazima awape polisi gari la bei kubwa.
Makonda ameahidi kuanzia Julai mpaka Desemba, atatoa Sh120 milioni kuwawezesha watoto wa kimaskini wanaoumwa moyo ili wafanyiwe upasuaji katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI). Kwa wastani, kila mwezi atatoa Sh10 milioni.
Mwezi wa Ramadhani Makonda alifuturisha walemavu kwa namna ya kifahari kabisa. Aligawa bidhaa za kutengenezea futari kwa maelfu ya watu. Na hayo ndiyo yamekuwa maisha ya Makonda, kunyoosha mkono na kusaidia watu mbalimbali, wagonjwa, walemavu, maskini na makundi mengine.
Kwenye hafla ya kuichangia Yanga, Waziri Mkuu alitoa mchango wa Sh10 milioni. Makonda alitoa uwanja Kigamboni ambao bila kuumiza kichwa, thamani yake ni kubwa kuliko Sh10 milioni za waziri mkuu.
Hivi mshahara wa Makonda ni tofauti na wakuu wa mikoa wengine? Maana kwa mshahara wa mkuu wa mkoa peke yake, hawezi kutoa na kusaidia kama anavyofanya.
Yapo mengi Makonda ameyafanya kuthibitisha utoaji wake. Swali ni hili; fedha na rasilimali ambazo anatoa, kama ni za Serikali, mbona wakuu wa mikoa wengine hawatoi kama atoavyo yeye? Tuseme yeye ni mkarimu kuliko wenzake?
Je, Makonda ni mjanja sana, kwa hiyo hutumia vizuri Bajeti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kufanya anayoyafanya?
Au kuna tofauti kubwa ya bajeti kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine? Kama ni hivyo, mbona wakuu wa mikoa wa Dar waliotangulia hawakuwahi kuwa na kasi ya utoaji kama aliyonayo Makonda?
Vipi Makonda ni tajiri mwenye pesa nyingi, kwa hiyo anatumia rasilimali zake binafsi? Ikiwa ukweli upo hivyo, tunapaswa kujiuliza, je, anatoa kwa ukarimu wake tu au kuna namna anataka afanye mbele ya safari ili kurejesha rasilimali zake anazotumia? Atarejesha zenyewe pekee au ataongeza na faida? Kama anatoa kwa ukarimu bila kutarajia chochote, tumpongeze kwa moyo wake.
Hivi sheria Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 inaruhusu kiongozi kugawa fedha nje ya kipato chake bila kuhojiwa.
Mwananchi
Tags