By THOMAS NG'ITU
MAMILIONI ya fedha yameingiza kwenye akaunti ya Yanga, baada ya wadau mbalimbali waliokuwa wameahidi kuipa timu hiyo pesa kuanza kutoa.
Katika hafla yao ya Kubwa Kuliko iliyoandaliwa na klabu hiyo hivi karibuni wadau mbalimbali waliahidi kuipa pesa timu hiyo ili iweze kujiendesha.
Pia wanachama wamekuwa wakichanga wenyewe kwa wenyewe kuhakikisha wanaisaidia timu hiyo kujiendesha ambapo walianza msimu uliopita.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msola alisema katika watu ambao wameahidi kutoa pesa wamepokea pesa kutoka Kampuni ya GSM Mall pamoja na mfanyabiashara maarufu nchini Rostam Aziz.
"Wapenzi na wanachama wa Yanga wwanatakiwa kutambua kwamba zile ahadi zimeanza kutimizwa na mpaka sasa tumeanza kupokea pesa kutoka GSM na Rostam kama vile ambavyo waliahidi," alisema.
Kampuni ya GSM iliahidi Sh 300 milioni wakati Rostam yeye akiahidi Sh 200 milioni ambapo jumla ya ahadi ziliztolewa kwenye hafla hiyo ni Sh 920 milioni.