Marufuku Kutumia Majina ya Watoto wa Kardashian na Kanye West..La Sivyo Unalo Babu


Dar es Salaam. Siku chache baada ya wanandoa mastaa, Kim Kardashian na Kanye West kutangaza kusajili majina ya watoto wao na kuyazuia yasitumike kibiashara, wanasheria wamesema kwa Tanzania, hilo linaweza kufanyika kwa majina ya kipekee.

North, Saint, Chicago na Psalm ni majina ya watoto hao yaliyosajiliwa na kuzuiwa kutumika katika biashara za vinywaji, vipodozi, mavazi au vinginevyo kwa kuwa ni mali ya familia na kwenda kinyume na katazo hilo ni kutangaza vita ya kisheria na familia hiyo na kwa kuwa ina hatimiliki ya majina hayo.

Kilichowashtua wengi ni ukawaida wa majina hayo, huku yakiwa tayari yameshatumika kwa namna nyingine kabla ya wao kuwapa watoto wao.

North lina maana ya kaskazini, Saint ni mtakatifu wakati Chicago ni mojawapo ya majimbo nchini Marekani na Psalm ni kitabu cha Zaburi kilichopo ndani ya Biblia.

Akizungumza na Mwananchi jana, wakili Jebra Kambole alisema sheria ya Tanzania inampa mtu mamlaka ya kusajili jina la kipekee na kulizuia lisitumike kwenye biashara ya mtu mwingine.

Alisema: “Tuna sheria ya usajili lakini hii inahusisha usajili wa kibiashara. Mfano, msanii anaweza kutumia jina lake kama brand na kulisajili kuzuia mwingine asilitumie.

“Inawezekana Marekani sheria yao inaruhusu hayo lakini hapa kwetu utasajili kama jina la alama ya biashara na linatakiwa kuwa la kipekee sio yale majina yanayofanana, mfano Diamond Platnumz anaweza kulisajili jina hilo kuwa mali yake na kuwazuia wengine kulitumia,” alisema Kambole.

Hoja ya Kambole haikutofautiana na iliyotolewa na mwanasheria Hamza Jabir aliyeeleza kuwa usajili unaweza kufanyika kwa majina ya kipekee.

“Jina linapokuwa la kawaida kila mtu anaweza kulitumia na huwezi kuzuia kwa namna yoyote. Ila kama jina ni la kipekee mfano Kisengo Safari Tours unaweza kulisajili,” alisema.

Habari zaidi kuhusu undani wa Kim Kardashian na mumewe Kanye West, kujimilikisha majina ya watoto wao, Soma Jarida la Starehe lililomo ndani.

By Elizabeth Edward, Mwananchi eedward@mwananchi.co.tz
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad