Michango ya Wabunge ya kuchangia maoni mbalimbali juu ya bajeti kuu ya Serikali imeendelea bungeni jijini Dodoma ambapo mbunge wa Kahama mkoani Shinyanga,Jumanne Kishimba maarufu kwa jina Prof.Kishimba ameitaka serikali kufuta tozo la Maiti kwenye chumba cha kuhifadhia maiti [Mortuary]
Mhe.Kishimba ameshangaa kufuta na kusamehe tozo kwenye unga wa ngano huku tozo la Maiti kwenye Mortuary ambayo ni Tsh.Laki tano ikiwa inaendelea hivyo ameishauri serikali kurudisha tozo ya keki na kuweza kufuta tozo ya maiti.
Mhe.Kishimba amesema ni jambo la kushangaza kwa watu wanaofariki kwa waganga wa jadi hawadaiwi bili yoyote na hupewa huduma ikiwa ni pamoja na sanda lakini mtu anapofariki akiwa hospitalini anadaiwa bili kubwa hivyo ni vyema serikali ikaangalia upya suala hilo kwani hali hiyo husababisha baadhi ya maiti hukosa ndugu wa kuichukua hospitalini kwa kukwepa kulipa bili na tozo ya Mortuary kutokana na hali ngumu ya Maisha na kusababisha kuzikwa ovyo.
“Mnajua waheshimiwa wabunge sisi ni marehemu watarajiwa ,kasoro itakuwa muda,tarehe na wakati,tumesamehe tozo ya keki lakini kwenye tozo ya maiti inabaki palepale,haiwezekani mtu apoteze mtu halafu atozwe bili na fedha ameitoa wapi”Amesema.
Mbunge Kishimba amesema yawezekana watengeneza Bajeti wanaishi Osterbay hawajui hali ngumu za watanzania kwa kufuta tozo ya keki ambayo kwa watanzania walio wengi amedai haina tija kwao na hivyo kuna haja ya serikali kurudisha tozo hiyo na kufuta tozo ya Maiti kwenye Mortuary.
Aidha ,Mhe.Kishimba ameiomba serikali iruhusu wananchi pindi wanapoenda kutibiwa ikiwa hawana fedha waende na mifugo yao hospitalini kama dhamana ili kutibiwa haraka na kuokoa Maisha yao kwani bado kuna dhana ya baadhi ya jamii kanda ya ziwa kutokuwa na uelewa juu ya bima kwani hudhani kuwa kukata bima ni kujitakia ugonjwa au kifo na elimu inatakiwa itolewe zaidi.
Sambamba na hayo,Mhe,Kishimba amesema kuna haja kubwa ya serikali kupunguza tozo za X-RAY ili watu wengi wanunue na kupekeka hospitalini hali itakayosaidia kupata huduma za X-Ray kwa bei nafuu.