Mjumbe mkuu wa Marekani nchini Afrika anaelekea Sudan wakati kukishuhudiwa mgogoro, idara ya mambo ya nje imesema.
Tibor Nagy, naibu waziri wa Afrika, "ataomba kusitishwa mashambulio dhidi ya raia".
Kumekuwa na mgomo wa kitaifa wa wafanyakazi, ulioanza siku ya Jumapili kuishinikiza serikali ya kijeshi kutoa fursa kuwepo kwa serikali ya kiraia.
Watu wanne wameuawa katika siku ya kwanza ya mgomo huo baada ya vikosi vya usalama kufyetua gesi ya kutoa machozi na risasi za moto.
Wizara ya mambo ya nje imesema Bwana Nagy 'ataziomba pande husika kushirikiana katika kuidhinisha mazingira' ya kuweza kuendeleza mazungumzo ya pande hizo mbili.
Ataijadili hali pia na waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ambaye amekuwa akijaribu kuwa mpatanishi kati ya baraza la kijeshi na upinzani Sudan, kabla ya hapo baadaye kuelekea Msumbiji na Afrika kusini.