Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amemwelezea marehemu Mwalimu Julius Nyerere kama kiongozi muhimu zaidi aliyewahi kutokea kwenye historia za medani za kisiasa kwa Afrika
Museveni aliyasema hayo wakati wa ibada ya kuombea mchakato wa Baba wa Taifa kuwa mwenyeheri na hatimaye mtakatifu, ibada iliyohudhuriwa na mataifa mbalimbali wakiwamo Watanzania zaidi ya 500
Uganda imeitenga siku ya Juni Mosi ya kila mwaka kuwa siku ya Nyerere, kwa ajili ya kuombea mchakato wa kumfanya awe Mtakatifu, ibada hiyo ya misa takatifu hufanyika katika Kanisa la Watakatifu Mashahidi wa Uganda la Namugongo, Kampala, Uganda
Rais Museveni alisema kuwa yeye ni mtoto wa kwanza wa Mama Maria Nyerere na alipongeza juhudi za familia ya Nyerere kwa kuungana na wanahija wengine kutoka nchi za Kenya, DRC, Rwanda, Burundi, Nigeria na duniani kwa ujumla kuja kuombea mchakato huo wa Nyerere kuwa mtakatifu
Alisema suala hilo linapaswa kuwa la kihistoria, kiutamaduni na kisiasa, lakini zaidi kiuchumi kupitia kazi na michango aliyoitoa wakati wa uhai wake, na kwamba ikiwa bado kuna udhaifu mahali, wanapaswa kuelimishwa taratibu ili suala la mashahidi wa Uganda lieleweke na liwe na nguvu zaidi