Watu tisa wameuawa kwa kupigwa risasi leo baada ya jeshi la Sudan kujaribu kuwatawanya waandamanaji waliopiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum.
Sudan Proteste in Khartum (Getty Images/AFP/A. Shazly)
Vikosi vya usalama vilivyokuwa kwenye magari yaliyobeba bunduki vimetumwa kote katika mji mkuu, wakati waandamanaji wakiweka vizuizi na kuzifunga barabara za mji huo.
Kwa mujibu wa shirioka la habari la Ujerumani la DW, Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan ambayo inawaunga mkono waandamanaji awali iliandika kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa watu wengine watatu wameuawa kwa kupigwa risasi na baraza la kijeshi na kufikisha watano idadi ya vifo. Pia imeripoti kutokea idadi kubwa ya majeruhi.
Msemaji wa baraza la kijeshi Luteni Jenerali Shams El Din Kabbashi amesema uvamizi huo wa kijeshi uliwalenga wahalifu na kuwa waandamanaji wako salama.
Amesema kambi ya waandamanaji haijavunjwa. Kabasshi amesema vikosi vya usalama vilijaribu kuwatawanya wahalifu katika eneo la Colomboa karibu na kambi ya maandamano na ndiposa vurugu zikazuka. Ameongeza kuwa baraza la kijeshi bado linaunga mkono suluhisho la kisiasa na lipo tayari kurejea haraka iwezekanavyo kwenye meza ya mazungumzo kuhusu kuundwa kwa serikali ya kiraia.
Shariff Mohammed Osman ni msemaji wa upinzani nchini Sudan. “Haifai, sio vizuri na haikubaliki katika sheria zozote au kanuni zozote kwa wanajeshi wenye silaha nzito kuwakabili raia wasiokuwa na silaha, bila kujali vitendo walivyovifanya”.
Chama cha Wasomi cha Sudan – SPA ambalo ni kundi lililoanzisha maandamano hayo mwezi Desemba, kimesema sasa kuna jaribio hilo la jeshi kujaribu kuuvunja mkusanyiko huo wa waandamanaji unachukuliwa kuwa mauaji ya kinyama na kuwataka Wasudan kushiriki katika “uasi kamili wa kiraia” ili kuliangusha baraza la kijeshi.
Marekani na Uingereza zimetoa wito wa kusitishwa ukandamizaji huo dhidi ya waandamanaji, ambao wanawataka viongozi wa kijeshi waliomuondoa madarakani rais wa muda mrefu Omar al-Bashir wakabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.
Balozi wa Uingereza mjini Khartoum, Irfan Siddiq amesema alisikia milio ya risasi akiwa katika makazi yake. Ubalozi wa Marekani mjini Khartoum umesema kuwa mashambulizi ya vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji na raia wengine hayastahili na lazima yasitishwe.
Sudan Proteste in Khartum (Getty Images/AFP/A. Shazly)
The Alliance for Freedom and Change, kundi linalounda vuguvugu la maandamano hayo, limeitisha maandamano na mikutano ya Amani kote nchini humo na vizuizi kuwekwa barabarani zikiwemo za mji mkuu Khartoum.
Mazungumzo kati ya viongozi wa maandamano na baraza tawala la kijeshi yamevunjika, baada ya pande zote kushindwa kukubaliana kama serikali ya mpito inayopangwa inapaswa kuongozwa na kiongozi wa kijeshi au wa kiraia.