Post ya Bondia Antony Joshua Baada ya Kichapo yawa Gumzo Mtandaoni

PICHA hii ya bingwa wa zamani wa uzito wa juu mikanda ya WBA, WBO na IBF, Anthony Joshua 'AJ', dhidi ya bingwa mpya wa mikanda hiyo, Andy Ruiz, imevunja rekodi.


Ilipigwa ulingoni, Madison Square Garden, New York, muda mfupi baada ya refa kumaliza pambano raundi ya 7. Refa aligundua AJ amepoteza mouthguard, alipomuuliza ilipo, akasema hajui, na akawa kama aliyechanganyikiwa.


Kuona hivyo, refa alimaliza pambano na Andy akawa mshindi kwa TKO. Hilo limekuwa pambano la kwanza la AJ kupigwa katika historia ya boxing.


Refa aligundua AJ hana mouthguard mdomoni, akiwa ametoka kuangushwa mara ya pili. Kabla ya hapo, raundi ya tatu, AJ alipelekwa sakafuni mara mbili lakini alimudu kuendelea na mchezo. Jumla, AJ aliangushwa mara nne.


Wachambuzi na mabondia wakongwe, wametilia shaka afya ya AJ kama alikuwa sawa kwa pambano, zaidi wamelaumu benchi lake ya ufundi. Wapo wanaolaumu kwamba huwenda alichoshwa na vikao vingi vya kibiashara kuliko maandalizi ya mchezo ndiyo maana akajikuta akipokea kichapo cha kushangaza.


Raundi ya tatu, AJ ndiye alianza kumdondosha Andy, baada ya hapo Andy alijibu mapigo fasta kwa kumdondosha AJ kisha ampeleka tena sakafuni mara ya pili. Kuanzia hapo AJ alionekana kuelemewa mpaka raundi ya 7.


AJ amekataa lawama za kupigwa apewe mwingine. Ametaka alaumiwe yeye. Zaidi akapongeza kuwa alipoteza pambano dhidi ya bondia bora.


Akaposti picha hiyo kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, akaandika "Ni usiku wa Andy. Hongera bingwa." Akaambatanisha na bendera ya Mexico. Yes, Andy ni Mmarekani mwenye asili ya Mexico.


Posti hiyo ya AJ imevunja rekodi kwa kupata likes, comments na shares nyingi mitandaoni. Sababu ni ule uungwana wa kimichezo aliounesha. Kukubali kupigwa na kumpongeza mshindi ndiyo darasa la uanamichezo katika boxing ambalo AJ amelitoa na kufurahisha wengi.


Kwa posti hiyo, AJ ameongeza mashabiki badala ya kupoteza. Ameahidi rematch dhidi ya Andy. Je, atasahihisha makosa kama Lennox Lewis alivyorudisha ubingwa wake kwa Hasim Rahman Novemba 2001?


Ndimi Luqman MALOTO  

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad