Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Mohammed Abdallah Mtonga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Mtonga anachukuwa nafasi ya Dkt. Omari Rashid Nundu ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania.
Uteuzi wa Dkt. Omari Rashid Nundu katika nafasi hiyo unafuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Bharti Airtel International juu ya uendeshaji wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania anapaswa kuteuliwa na Serikali ya Tanzania.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo Afisa Mkuu wa Ufundi (Chief Technical Officer – CTO) pia anateuliwa na Serikali ya Tanzania, na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo ni Dkt. Prosper Godfrey Mafole.
Wajumbe wengine watakaoiwakilisha Serikali katika Bodi ya Airtel Tanzania ni John Marato Sausi na Lekinyi Ngariapusi Mollel.