Rais Magufuli Atoa Agizo TRA Kumlipa Fidia Mfanyabiashara Aliyezuiliwa Bidhaa Zake Tangu 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kumlipa fidia mfanyabiashara ambaye bidhaa zake zilishikiliwa na Mamlaka hiyo tangu mwaka 2015 kinyume na taratibu.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo, wakati akiongea na wafanyabiashara kutoka wilaya zote za Tanzania kwa lengo la kuangalia changamoto na fursa zilizopo katika kufanya biashara nchini.

Ametoa maagizo hayo baada ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa kuelezea namna alivyoingilia kati suala la mfanyabiashara huyo wa Kariakoo (jina lake halikujulikana mara moja) kurejeshewa bidhaa zake zilizokuwa zimezuiliwa baada ya mfanyabiashara huyo kukataa kutoa rushwa kwa Maafisa watatu wa TRA.

“Hao watatu wote Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kawashike na uwaweke ndani halafu wapelekwe Mahakamani, wakiwa Mahakamani Kamishna Mkuu wa TRA uwe umewasimamisha kazi, lakini TRA mkapige hesabu ile biashara yake imekaa kwa miaka mitatu mkamlipe fidia,” Rais Magufuli alitoa maagizo.

Aidha, Rais amewataka wafanyabiashara kuiga mfano wa mfanyabiashara mwenzao aliyekataa kutoa rushwa na kuwaomba watoe ushirikiano katika kulipa kodi na pia Mamlaka ya Mapato kutomuonea mfanyabiashara katika kumkadiria kodi.

Waziri Mkuu alikuwa akielezea malalamiko aliyopata kutoka kwa wafanyabiashara hususani kodi kubwa na rushwa ambapo baadhi ya maofisa wamekuwa wakitumia vibaya majina ya viongozi kwa kusingizia kuwa ni maagizo kutoka juu.

Kassim Majaliwa alieleza kwamba aligundua matatizo hayo baada ya kutembelea eneo la biashara la Kariakoo jijini Dar es Salaam na kugundua mfanyabishara mmoja aliingia na bidhaa kutoka Zambia na kuwa na vibali vyote lakini alipofika Kimara alizuiliwa na kuomba rushwa lakini Mfanyabiashara huyo alikataa kutoa rushwa na TRA wakachukua bidhaa zake kupeleka bohari.

Kwa upande wake Waziri Mkuu amewataka wafanyabishara kuendelea kuwa na imani na Serikali ina haki na wajibu wa kuwalinda wafanyabishara kwa namna yeyote ile na ndio maana Serikali inachukua hatua mbalimbali ili kuweka mazingira bora kwa wafanyabishara.

Majaliwa alisema kuwa Serikali itahakikisha inajenga mazingira wezeshi nchini na pia itaimarisha biashara za mipakani na pia eneo la Kariakoo ambalo ndio soko kubwa ambapo wafanyabishara kutoka Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekuwa wakichukua bidhaa Kariakoo.

Mkutano wa Rais na wafanyabiashara kutoka wilaya zote mchini uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam pia ulihudhuriwa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi, Mawaziri, Makatibu Wakuu na baadhi ya Wakuu wa taasisi za Serikali na sekta binafsi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad