Rais Trump Akutana na Kim Jong-un
0
June 30, 2019
Rais Donalad Trump wa Marekani amekutana na kiongozi wa Korea Kaskazini katika eneo lisilo la kijeshi la mpaka wa Korea mbili ambapo viongozi hao wawili walipeana mikono kuonesha ishara ya matumaini ya amani.
Huu ni mkutano wa tatu kwa viongozi hao wawili katika kipindi cha mwaka mmoja. Kukutana kwa viongozi hao kumeongeza matumaini ya kuyarejesha mezani mazungumzo ya nyuklia yaliokwama.
Rais Trump aliandamana na Kim kuvuka eneo hilo la mpaka lisilo la kijeshi na ambalo kwa miaka kadhaa limekuwa katika fukuto la Vita Baridi.
Trump ndiye Rais wa kwanza wa Marekani aliye madarakani kukanyaga eneo hilo la upande wa ardhi ya Korea Kaskazini.
Baada ya mazungumzo ya takribani dakika 50 Trump na Kim walirejea upande wa Korea Kusini na kuungana na Rais Moon Jae-in kwa mazungumzo mafupi.
Baadae Trump na Kim walifanya mazungumzo ya faragha.
Trump aliwasili Korea Kusini jana jioni kwa ajili ya mazungungumzo na Moon baada ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa mataifa 20 yalioendelea kiviwanda duniani huko Osaka, Japan, ambapo alifanya ziara ya kushtukiza na kutoa wito wa kutaka kuonana na Kim na hatimae jambo hilo kufanikiwa.
Tags