Serikali imesema kuwa kati ya kipindi cha mwaka 2013 hadi Mei 2019 imetaifisha mali za wahalifu zenye thamani ya Tsh. Bilioni 93.16 zilizokamatwa kwenye sekta za Madini, Maliasili na Sekta ya fedha (Upatu) ikiwa ni sehemu ya kudhibiti uhalifu kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Uhalifu huo unaodaiwa kukithiri katika miaka ya nyuma na ambao sasa unaendelea kudhibitwa unatajwa kuliingizia Taifa hasara ya Mabilioni ya fedha, hatua iliyoifanya Serikali kuudhibiti kwa kutaifisha mali za wahusika wa uhalifu huo.
Hayo yalibainishwa leo (Jumatano Juni 12, 2019) Jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati akifungua mkutano wa maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Urejeshaji wa Mali Zinazohusiana na uhalifu wenye jumla ya nchi wanachama 16.
Samia alisema hivi sasa Serikali ya Tanzania inapanga mikakati ya kuondokana kabisa na uhalifu huo kutokana na sera ya kudhibiti Rushwa pamoja na kuanzisha mahakama maalum zitakazoshughulikia ufisadi Nchini Tanzania.
“Sisi Tanzania tunaimarisha Sera zetu za kupambana na Rushwa na Ufisadi, tunaenda sambamba na umoja wetu huu wa ARINSA hivyo tunazishauri nchi zingine ambazo zipo kwenye umoja huu na bado hazijatunga Sera na Sheria ziharakishe mchakato ili twende sawa” alisema Samia.
Kwa upande wake Waziri wa Sheria na Katiba, Balozi Augustine Mahiga alisema mkutano huo pamoja na mambo mengine utazungumzia mikakati ya pamoja ya kudhibiti uhalifu wa mipakani hasa kwenye udhibiti wa uingizwaji wa bidhaa haramu ikiwepo dawa za kulevya.
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Biswalo Maganga alisema mkakati wa kutaifisha mali za wahalifu umekuja kufuatia kuona vifungo gerezani kwa wahalifu hao havitazinufaisha nchi hizo na badala yake kuchukua mali zao ili kukomesha kabisa suala hilo.
Aidha alisema tayari wataalamu kadhaa wa upelelezi wa kufuatilia mali na kuzitaifisha wameshapata mafunzo na kwamba zoezi hilo linaendelea ili kuhakikisha linafanyika kikamilifu na kwa usiri mkubwa.
ARINSA ni umoja wa urejeshaji wa mali zinazohusiana na uhalifu wenye Nchi wanachama 16 zilizopo Barani Afrika ambao kwa pamoja wanakusudia kukabiliana na uhalifu hususan kwenye mipaka ya nchi hizo.
Serikali Yataifisha Mali Za Wahalifu Zenye Thamani Ya Tsh Bilioni 93.16
0
June 12, 2019
Tags