Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuanzia mwezi Januari hadi Juni 19 mwaka huu, jumla ya wagonjwa 4,320 na vifo vinne vilivyotokana na homa ya dengue vimetolewa taarifa
“Mkoa wa Dodoma wagonjwa walikuwa watatu na kifo kimoja. Tanga wagonjwa 207, Pwani 57, Morogoro 16, Arusha wagonjwa watatu, Singida wawili, Kagera pia wawili. Vifo vimetokea katika hospitali ya rufaa Dodoma na Dar es Salaam katika hospitali ya Hindu Mandal na Regency,” amesema Ummy.
Akizungumzia kuhusu changamoto, Ummy amesema ya kwanza ni gharama za kupima. Amesema Ingawa Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imenunua vipimo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji na kuviuza kwa bei nafuu ikilinganishwa na gharama inayotozwa kwenye baadhi ya hospitali binafsi, bado wananchi wanashindwa kumudu gharama za uchangiaji matibabu ya ugonjwa huu.
Pia amesema jamii haijaweza kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kampeni ya usafi wa mazingira ambayo ni njia kuu ya kudhibiti mazalia ya mtu na watoa huduma za afya hawafuati kikamilifu miongozo ya matibabu ya ugonjwa huu.