Tanzania yapatiwa Tsh. Bilioni 60 za msaada kutoka China

Tanzania imetia saini mkataba wa kupatiwa fedha za msaada wa Sh60 bilioni kutoka Serikali China bila ya masharti yeyote ambapo Serikali ya Tanzania itaamua matumizi yake katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wake.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Juni 24, 2019 na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Beijing China imesema mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Palamagamba Kabudi aliyeiwakilisha Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la China Zhou Liujun kwa upande wa China.

Mkataba huo umesainiwa punde tu mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya Waziri Kabudi na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi.

“Mazungumzo ya mawaziri hao yalilenga kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya China na Tanzania sambamba na kuibua maeneo ya kipaumbele na kimkakati yatakayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya nchi hizo,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia imetaja maeneo yatakayopewa kipaumbele kuwa ni pamoja na upembuzi yakinifu kwa ajili ya upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ili kuwa Taasisi Mahiri ya Tiba ya Moyo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mengine ni ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme ya Ruhudji (megawatt 358) na Rumakali (megawatt 222) mkoani yaliyoko mkoani Iringa na Njombe ambayo yote kwa pamoja yatakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa takribani megawati 580,pamoja na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge railway) sambamba na ukarabati wa reli ya Tazara.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad