Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema imeunda kikundi maalumu kinachoshirikisha watoa huduma za mawasiliano ili kuharibu simu za matapeli wanaotuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS).
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo, katika mkutano wa wadau wa sekta ya mawasiliano, uliolenga kupokea kero na mapendekezo juu ya utendaji wa mamlaka hiyo.
Mihayo alisema suala la SMS za utepeli kutumwa kwa watu limekuwa sugu, hivyo TCRA na kampuni za mawasiliano, walikaa na kuunda kikundi cha kushughulikia namba za simu zinazotuma ujumbe wa utapeli.
“Moja ya malalamiko sugu katika suala la mawasiliano ni watu kutumiwa ujumbe wa utapeli, wametapeliwa sana, wapo wanaolalamika kupata ujumbe usiku na kusababisha mgogoro katika ndoa, lakini kama TCRA na watoa huduma tukaamua kuunda ‘group’ letu la kuwashughulikia watu wa namna hiyo.
“Katika ‘group’ hilo, mmoja wapo akipokea ujumbe wa utapeli ukiwamo kutuma pesa katika namba fulani, sisi watu wa mawasiliano na watoa huduma tunashirikiana kuharibu ile namba na simu husika, nadhani SMS zimepungua kwenu, tunaomba wale wanaotumiwa ujumbe huo watumie namba hiyo katika kampuni husika.
“Naombeni wananchi kuweni makini, ukitumiwa ujumbe wowote kaa kimya, inakuwaje unatuma fedha kwa mtu ambaye humjui?.
TCRA yaunda kikundi maalumu kuharibu laini za watuma SMS za kitapeli
0
June 15, 2019
Tags