Timu Ya Wizara Ya Kilimo Yawasili Kanda Ya Ziwa Kubaini Changamoto Za Zao La Pamba

Uongozi wa Wizara ya Kilimo umewasili katika mikoa ya Kanda ya ziwa ili kubaini changamoto zinazowakabili wakulima wa zao la Pamba na kuzitafutia ufumbuzi.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameongoza timu hiyo ambapo amezuru katika mikoa ya Tabora na Simiyu kwenye Wilaya za Igunga na Meatu.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) anatembelea katika Mikoa ya Shinyanga na Mara huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akizuru katika Mikoa ya Geita na Mwanza.

Akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Imalanguzi Kijiji cha Igurubi Wilayani Igunga, na Kijiji cha Mwabuzo Wilayani Meatu, Mhe Hasunga amesema kuwa wizara ya Kilimo ipo katika mchakato wa kutafuta mfumo madhubuti wa ununuzi wa Pamba.

Alisema mfumo huo punde utakapoelekezwa utatumika lakini ni mfumo ambao utakuwa maalumu kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha sekta ya pamba nchini.

Amesisitiza kuwa ili kuimarisha kilimo nchini ni wazi kuwa wakulima wanapaswa kupatiwa Pembejeo za kilimo ambazo ni Mbegu, Mbolea na Viuatilifu. “Hatuwezi kuwakomboa wakulima kama tutaendelea na uagizaji wa pembejeo feki ambazo zinawarudisha nyuma wakulima” Alikaririwa Mhe Hasunga

Katika ziara hiyo yenye lengo la kutambua changamoto ya zao la Pamba, masoko yake na upatikanaji wa pembejeo, Waziri Hasunga ameeleza kuwa zao la pamba ni sehemu ya mazao makuu ya biashara nchini hivyo ni lazima litafutiwe ufumbuzi.

Aidha, Mhe Hasunga ametumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi katika mikutano hiyo kuwa Wizara ya Kilimo ipo katika mapitio ya sera ya Kilimo ya mwaka 2013 itakayopelekea kuwa na sheria ya kilimo itakayomnufaisha mkulima na kulinda rasilimali za kilimo ikiwemo ardhi.

Kadhalika, amesema kuwa serikali inaendelea na zoezi la usajili wa wakulima huku akisisitiza umuhimu wa sekta ya umwagiliaji ambayo ikisimamiwa vizuri itakuwa muarobaini wa kilimo pasina kutegemea msimu wa mvua kwa ajili ya kilimo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad